Viongozi wa dini kutoka mikoa ya Nyanda za Juu Kusini wamewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kushiriki Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025, huku wakisisitiza umuhimu wa kudumisha amani kabla, wakati na baada ya uchaguzi huo.
Viongozi hao kutoka mikoa ya Mbeya, Iringa, Njombe, Songwe na Rukwa wametoa kauli hiyo leo Oktoba 23, 2025, katika Kongamano la Amani na Uchaguzi lililofanyika jijini Mbeya, likiwa na kauli mbiu “Kupiga kura ni haki yetu na kulinda amani ni wajibu wetu.”
Mwishoni mwa kongamano hilo, viongozi wa dini walitoa tamko la maazimio, likisisitiza ulinzi wa amani ya nchi na kuhimiza wananchi kushiriki kwa wingi katika uchaguzi huo.
Akisoma tamko hilo, Askofu Profesa Donald Mwanjoka, Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la TAG ICC Mbeya, alisema maazimio hayo yanawakumbusha Watanzania wote waliojiandikisha kuhakikisha wanajitokeza kupiga kura, kufanya maamuzi ya busara na kuchagua viongozi waadilifu watakaoitumikia nchi kwa uaminifu.




“Kushiriki katika Uchaguzi ni haki ya kikatiba na wajibu wa kizalendo. Amani ni msingi wa maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kiroho, hivyo tofauti za kisiasa hazipaswi kuwa chanzo cha chuki, maandamano au vurugu,” alisema Prof. Mwanjoka kwa niaba ya Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT) na Kamati za Amani za mikoa hiyo.
Viongozi hao pia waliitaka Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru, haki na wa kuaminika, huku vyombo vya ulinzi na usalama vikitakiwa kuzingatia utu, sheria na haki za binadamu katika utekelezaji wa majukumu yao.
Kwa upande wake, Sheikh Msafiri Njalambaha, Sheikh wa Mkoa wa Mbeya na Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Amani ya Mkoa huo, alisema amani ni nguzo kuu ya maisha ya ibada na ustawi wa taifa.




“Hakuna uchaguzi, maendeleo wala ibada bila amani. Kura ni haki yetu, amani ni wajibu wetu,” alisema.
Askofu Oscar Ongele, Mwenyekiti wa JMAT Mkoa wa Mbeya, aliwataka viongozi wa dini kutumia nyumba za ibada kuhamasisha waumini waliojiandikisha kwenda kupiga kura kwa amani na bila hofu.
“Tujitokeze kwa wingi, tuwahimize waumini wetu washiriki bila hofu, vyombo vya ulinzi vipo kulinda amani yetu,” alisema.
Kutoka mkoani Iringa, Dk. Joseph Mgumi, Mwenyekiti wa Kamati ya Amani ya mkoa huo, alisema hakuna maendeleo bila uongozi na hakuna uongozi bila uchaguzi, hivyo ni muhimu kila Mtanzania kushiriki.
“Tupige kura kwa wingi ili tupate viongozi watakaotuletea maendeleo,” alisema.




Sheikh Alhaj Batuza wa Mkoa wa Songwe alisisitiza kuwa amani ndiyo msingi wa kila jambo.
“Wazee wetu walihangaika kuupata uhuru, leo sisi tunapaswa kuilinda amani kwa vitendo, si kwa maneno,” alisema.
Naye Askofu Mstaafu Ambele Mwaipopo wa KKKT Dayosisi ya Ziwa Tanganyika (Rukwa) aliwakumbusha wananchi kuwa ni wajibu wa kila mmoja kulinda amani aliyopewa na Mungu.
“Asicheze mtu na amani ya taifa letu; kila mmoja awe mlinzi wa amani,” alisema.
Kwa upande wa Mkoa wa Njombe, Sheikh Shabani Dinga, alisema Watanzania wanapaswa kujitokeza kupiga kura kwa amani, huku wakionesha uvumilivu na ukomavu wa kisiasa.
Askofu Jacob Kahemele wa Kanisa la Anglikana Mbeya alisema tofauti za kisiasa hazipaswi kugawa watu.
“Uchaguzi ni mchakato wa kawaida wa kidemokrasia. Tuwe na hekima, tuvumiliane, tushiriki kwa amani,” alisema.
Aidha, Askofu Erica Mwakyokile wa Kanisa la Pentecost Shilo Mkoa wa Mbeya aliwataka Watanzania kuendelea na maombi hadi Uchaguzi utakapomalizika kwa amani.
“Kila mtu yuko hapa kwa sababu ya amani, tuendelee kuomba ili Tanzania iendelee kuwa nchi ya utulivu,” alisema.
Viongozi hao kwa pamoja walihitimisha kwa kuwataka Watanzania kutambua kuwa kura moja inaweza kuandika historia mpya ya taifa, hivyo wajitokeze kupiga kura kwa amani, umoja na uzalendo, wakiweka mbele maslahi ya nchi kuliko ya mtu binafsi.





