Saturday, November 8, 2025
spot_img
HomeBiasharaWafanyabiashara Shinyanga wapongeza utulivu, walalamikia kupanda kwa bei ya bidhaa

Wafanyabiashara Shinyanga wapongeza utulivu, walalamikia kupanda kwa bei ya bidhaa

Wafanyabiashara katika Soko Kuu la Mjini Shinyanga wameendelea kufanya shughuli zao za kibiashara kama kawaida, licha ya kulalamikia baadhi ya bidhaa muhimu kama viazi mviringo kuadimika na kuuzwa kwa bei ya juu.

Wakizungumza leo Novemba 5, 2025, wamesema hali ya biashara imeanza kurejea taratibu baada ya serikali kutangaza kurejea kwa utulivu kufuatia vurugu zilizojitokeza wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29.

Mfanyabiashara Ayoub Amosi amesema wanamshukuru Serikali kwa kurejesha hali ya amani, jambo lililowapa fursa ya kuendelea na biashara zao kwa utulivu bila hofu, ingawa changamoto ya upatikanaji wa baadhi ya bidhaa bado ipo.

“Tunaishukuru Serikali kwa kurejesha hali ya amani hapa nchini. Sasa hivi wateja wanakuja kwa wingi tofauti na kipindi cha vurugu wakati wa uchaguzi ambapo biashara zilidorora kabisa,” alisema Amosi.

Kwa upande wake, Monica Charles, mfanyabiashara wa samaki wa kukaanga, alisema kipindi ambacho soko lilikuwa likifungwa kabla ya muda, walikumbwa na hasara kutokana na bidhaa zao kuharibika kabla ya kuuzwa.

“Samaki walikuwa wanaoza kwa sababu hatukuwa tunauza vizuri. Tunashukuru hali imetulia, biashara zimerudi,” alisema.

Makamu Mwenyekiti wa Soko, Wiliamu Nyaingi, ameiomba serikali kuendelea kuimarisha ulinzi na kudumisha amani, akisisitiza kuwa mazingira salama ni muhimu kwa maendeleo ya shughuli za kiuchumi.

Nao baadhi ya wateja akiwamo Ashura Khamisi, wamepongeza juhudi za serikali kurejesha utulivu na kusema sasa wanafika sokoni bila hofu kupata mahitaji yao ya kila siku.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, amethibitisha kuwa hali ya usalama imeimarika na shughuli za kiuchumi zinaendelea kama kawaida katika maeneo yote ya mkoa huo.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments