Saturday, November 8, 2025
spot_img
HomeElimuMkurugenzi Nyange akabidhi mashine ya kudurufu kwa Shule ya Sekondari Tandika

Mkurugenzi Nyange akabidhi mashine ya kudurufu kwa Shule ya Sekondari Tandika

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara-Mikindani, Mwalimu Hassan Nyange, ameendelea kutekeleza ahadi zake za kuboresha sekta ya elimu kwa kukabidhi mashine ya kudurufu (photocopy machine) katika Shule ya Sekondari Tandika, mkoani Mtwara.

Hafla ya makabidhiano hayo imefanyika shuleni hapo na kuhudhuriwa na viongozi wa elimu, walimu, pamoja na wanafunzi, ambapo wadau wa elimu wamempongeza Mkurugenzi Nyange kwa hatua hiyo, wakieleza kuwa ni kielelezo cha uongozi makini na wenye kujali maendeleo ya sekta ya elimu.

Akizungumza wakati wa makabidhiano, Mwalimu Nyange alisema hatua hiyo ni sehemu ya mpango wa halmashauri kuboresha miundombinu na mazingira ya kufundishia na kujifunzia katika shule za manispaa hiyo.

“Mashine hii inalenga kurahisisha kazi za walimu, hasa katika uchapaji wa mitihani na nyaraka za kitaaluma. Hii itaongeza tija na ufanisi katika ufundishaji,” alisema Nyange.

Aidha, aliwataka walimu na uongozi wa shule kuhakikisha kuwa mashine hiyo inatunzwa na kutumika kwa malengo ya kitaaluma pekee, akisisitiza kuwa ni mali ya umma inayopaswa kuhifadhiwa kwa uangalifu ili idumu na kuwanufaisha vizazi vijavyo.

Kwa upande wake, Afisa Elimu Sekondari wa Manispaa ya Mtwara-Mikindani, Mangula Mayemba, alisema mashine hiyo imenunuliwa kwa kutumia fedha za mapato ya ndani ya halmashauri, ikiwa ni sehemu ya juhudi za serikali za mitaa katika kuboresha huduma za kijamii, hususan elimu.

“Shule nyingi zimekuwa zikikabiliwa na changamoto ya uchapaji wa mitihani, lakini msaada huu utapunguza gharama na muda uliokuwa ukitumika kwa kazi hizo,” alisema Mayemba.

Aliongeza kuwa uwepo wa mashine hiyo utachochea ari ya walimu kufundisha kwa bidii na hatimaye kuleta matokeo bora katika ufaulu wa wanafunzi.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments