Katavi – Wizara ya Kilimo imeendelea kutekeleza majaribio ya kupunguza tatizo la tindikali kwenye udongo kupitia mpango wa Smart Fertility Subsidy, ambao unahusisha upimaji wa kiwango cha tindikali (pH) na uchukuaji wa majira nukta (coordinates) katika mashamba ya wakulima.
Majaribio hayo yalianza katika mikoa ya Njombe na Iringa, ambayo imebainika kuwa na kiwango kikubwa cha tindikali, na sasa timu ya wataalamu ipo mkoani Katavi ikiendelea na zoezi hilo. Wakulima kutoka vijiji 25 vya kata nane katika wilaya za Tanganyika na Mlele wanashiriki katika majaribio hayo ya ruzuku makini.
Wataalamu kutoka Idara ya Usimamizi na Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Kilimo wamekuwa wakitoa elimu kwa wakulima kuhusu namna ya kupima pH ya udongo na kutumia chokaa kilimo kama njia ya kupunguza tindikali.
Akizungumzia kuhusu utekelezaji wa mradi huo, Afisa Kilimo William Tsere, ambaye anaongoza timu ya wataalamu, alisema kuwa wakulima wameonesha ushirikiano mkubwa na wanashiriki kikamilifu katika majaribio hayo.

“Kazi imekuwa nzuri katika kata na vijiji vyote tulivyofikia. Tumewafikia wakulima 1,468, tukashirikiana na maafisa kilimo wa wilaya za Tanganyika na Mlele. Ushirikiano kutoka kwa wakulima wenyewe umekuwa wa kutia moyo,” alisema Tsere.
Majaribio haya yanafanyika kwa kipindi cha miaka mitatu (2025–2028) chini ya Programu ya Mifumo Himilivu ya Chakula (TFSRP), yakihusiana na kiashiria kidogo namba 7.2 (DLI 7.2) kinacholenga kufanya majaribio ya mbolea na visaidizi vya mbolea kwa ajili ya kupunguza tindikali kwenye udongo.
Mkulima Mandwa Msago kutoka Kijiji cha Mchakamchaka alisema amefurahia huduma hiyo baada ya shamba lake kupimwa na kupatiwa ushauri wa kitaalamu.
“Huduma hii imenisaidia kuelewa hali ya udongo wangu. Ushauri huu utanifanya niboreshe kilimo changu na kupata mazao bora zaidi. Nashukuru serikali kwa kufika hadi mashambani kwetu,” alisema Msago.




