Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF) limesema limejipanga kuhakikisha KMKM inaandika historia kwa kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza.
Kesho, KMKM itamenyana na Azam FC ya Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Amaan Complex, Zanzibar.
Katibu Mkuu wa ZFF, Hussein Ahmada, amesema mechi hiyo ni ya kihistoria na wanaiangalia kama jukumu la kitaifa.
“Tunataka mwaka huu Zanzibar iandike historia. Azam ni timu bora, lakini tumejipanga kupambana,” alisema Ahmada.
KMKM, chini ya kocha Hababuu Ali, ilisonga mbele baada ya kuzibwaga AS Port ya Djibouti na sasa inataka kuendeleza moto huo. Kikosi cha Azam kimewasili visiwani tayari kwa mchezo huo wa saa 10:15 jioni.




