📌 Waziri Dk.Gwajima amshukuru Rais Samia ahidi kushirikiana na Wazee.
‎
‎Na Saidi Saidi – WMJJWM, Dar es Salaam
‎
‎Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka Wazee kuendelea kuhamasisha amani ya nchi kwa kuwapatia vijana elimu ya uzalendo, kuwaongoza katika misingi ya maadili na kuwahimiza kuipenda na kuilinda nchi yao.
Rais Samia ameyasema hayo Desemba 2, 2025, wakati akihutubia Taifa na kuzungumza na wazee wa Jiji la Dar es Salaam katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam. Â




‎Aidha, Rais Dkt. Samia amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa wazee, ikijumuisha kuimarisha mifumo ya Ustawi wa Jamii na programu zinazolenga kuongeza upatikanaji wa huduma bora kwa wazee nchini huku akisema kuwa wazee wana mchango muhimu katika kuhifadhi misingi ya taifa, hivyo juhudi za kuboresha ustawi wao zinaendelea kupewa kipaumbele.
‎
‎Kwa upande wake, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, ambaye Wizara yake inasimamia masuala ya wazee kupitia ukurasa wake wa Instagram amepongeza na kuunga mkono wito wa Mhe. Rais Samia huku akisisitiza kuwa Wizara itaendelea kuweka mikakati madhubuti ya kuwawezesha wazee kushiriki kikamilifu katika mijadala na shughuli za kijamii.

Dkt. Gwajima ameeleza kuwa Wizara itaendeleza ushirikiano na Mabaraza ya Wazee nchini ili kuongeza utoaji wa elimu na kuwaweka karibu na vijana kwa lengo la kujenga vizazi vyenye maadili, uzalendo na umoja wa kitaifa.
‎
‎Nao wazee waliohudhuria mkutano huo wameahidi kuunga mkono maelekezo ya Mhe. Rais kwa kushirikiana na Serikali, jamii na taasisi mbalimbali katika kuhamasisha amani, kuelimisha vijana na kuwa mabalozi wa umoja na mshikamano katika maeneo yao huku wakieleza kuwa wako tayari kutumia uzoefu na hekima yao kuimarisha nchi na kuhakikisha misingi ya amani inaendelezwa kwa vizazi vinavyofuata.






