Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Tedros Adhanom Ghebreyesus, amemtunuku tuzo Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Doris Mollel, Doris Mollel, kwa kutambua uongozi wake na mchango mkubwa katika kuboresha afya na ustawi wa mama na watoto wachanga duniani, hususan nchini Tanzania.
Hafla hiyo imefanyika katika ofisi za WHO jijini Geneva, ambapo Dk. Tedros alimpongeza Doris kwa juhudi zake zisizochoka katika kuendeleza huduma za watoto wachanga, akisema kazi yake imekuwa na athari kubwa kitaifa na kimataifa.
Akizungumzia mafanikio ya hivi karibuni, Dk. Tedros alieleza kuwa kupitia juhudi za Doris, kituo maalum cha huduma kwa watoto wachanga (Neonatal Care Unit) kilizinduliwa mwezi uliopita katika Hospitali ya Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza. Kituo hicho kinatumia mfumo wa “Zero Separation”, unaolenga kutotenganisha mama na mtoto, kikihudumia watoto 42 kwa wakati mmoja, pamoja na vyumba maalum kwa ajili ya akina mama na maeneo ya kutembelea kwa baba.
Aidha, juhudi zake zimechangia mabadiliko muhimu ya sera nchini Tanzania, ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa muda wa likizo kwa wazazi wa watoto njiti, ujumuishaji wa watoto hao katika bima ya afya, pamoja na kujumuishwa kwa huduma za watoto njiti katika mitaala ya elimu.
Mbali na hilo, Doris ni kinara wa afya ya uzazi na anaongoza Muungano wa Haki za Afya ya Uzazi na Jinsia Tanzania, akihamasisha upatikanaji wa huduma bora kwa wanawake na watoto.
Katika ngazi ya kimataifa, ameendelea kuwa sauti muhimu ya kuhakikisha kila mtoto anapata mwanzo bora wa maisha. Pia alichangia kwa kiasi kikubwa kutambuliwa rasmi kwa World Prematurity Day kama siku muhimu ya kimataifa chini ya WHO.
Dk. Tedros alimshukuru Doris kwa kujitolea kwake, huruma na uongozi thabiti katika kulinda na kuendeleza afya ya wanawake na watoto duniani.




