Mafuriko makubwa yameendelea kusababisha maafa katika Kaunti ya Kisumu, ambapo zaidi ya familia 3,000 katika eneo la Nyakach zimelazimika kuhama makazi yao baada ya Mto Mirui kufurika.
Maafa hayo yamesababisha uharibifu wa takriban ekari 3,000 za mazao, huku wakazi wakilazimika kutumia boti kwa shughuli za uokoaji. Walioathirika wamehifadhiwa katika vituo vinane vya dharura vilivyoandaliwa na serikali.
Wakati huo huo, jijini Nairobi hali ni mbaya zaidi baada ya watu 37 kuripotiwa kufariki dunia. Mamlaka zimewaamuru wakazi wa mabondeni kuhama mara moja kutokana na hatari ya Bwawa la Nairobi kuvunja kingo zake.
Idara ya Hali ya Hewa imeonya kuwa mvua za wastani hadi kubwa zinatarajiwa kuendelea hadi Jumanne, na kuwataka wananchi kuchukua tahadhari ili kuepuka madhara zaidi kwa maisha na mali.




