Friday, May 15, 2026
spot_img
HomeHabariBodi za usuluhishi wa ndoa zatakiwa kulinda siri za wanandoa

Bodi za usuluhishi wa ndoa zatakiwa kulinda siri za wanandoa

Katika hatua inayolenga kujenga imani na kuongeza ufanisi katika kulinda siri za wanandoa, Bodi za Usuluhishi wa migogoro ya ndoa zimeaswa kutunza siri hizo ili kuondoa hofu kwa wanandoa kuogopa kupeleka migogoro yao.

Akifungua mafunzo hayo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Misenyi, Phocas Rwegasira  amesema wajumbe wa bodi wanapaswa kuwa waadilifu na kuhakikisha taarifa zote wanazozipata kutoka kwa wanandoa zinabaki kuwa siri kwa manufaa ya kulinda heshima na ustawi wa familia husika kwani uvujishaji wa siri unaweza kuongeza migogoro na kuondoa imani ya wananchi kwa bodi hizo.

Amesisitiza kuwa wajumbe wa bodi si mahakimu bali ni wasuluhishi wenye jukumu la kuleta maridhiano kwa kutumia mazungumzo yenye hekima, busara na usiri mkubwa, kwakuwa mazingira ya usuluhishi yanapaswa kuwa salama kwa wanandoa kueleza changamoto zao bila hofu ya taarifa zao kusambazwa katika jamii.

Aidha, amesema mafanikio ya bodi za usuluhishi wa ndoa hayawezi kupimwa kwa idadi ya mashauri yanayopokelewa pekee, bali kwa uwezo wa kurejesha amani ndani ya familia na kujenga mshikamano katika jamii. Hivyo familia nyingi zimekuwa zikivunjika kutokana na kukosekana kwa faragha na usimamizi mzuri wa migogoro ya ndoa.

Katika mafunzo hayo, wajumbe wamekumbushwa umuhimu wa kuzingatia maadili ya kazi, kutunza nyaraka za mashauri kwa usalama pamoja na kuepuka kutoa taarifa za wanandoa kwa watu wasiohusika. Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria imeeleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za kuimarisha taasisi ya ndoa na kulinda haki za familia nchini.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments