Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) pamoja na kutoa elimu na huduma kwa wanachama na wananchi wanaotembelea banda la Mfuko huo kwenye Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma kwenye viwanja vya Chinangali jijini Dodoma, pia unapita “Banda kwa Banda” ili kuwafikia wanachama wake na kuwahudumia.
Hayo yamesemwa na Afisa Uhusiano wa PSSSSF,Regina Kumba Juni 18, 2026, alipoongozana na maafisa wenzake wa PSSSF kwenye Maonesho hayo.
Amesema, ukiacha wananchi wanaotembelea maonesho hayo, asilimia kubwa ya wanatoa huduma kwenye mabanda mbalimbali ni wanachama wa PSSSF. “ Tunatambua kuwa watumishi walio kwenye viwanja hivi nao pia wanawahudumia wananchi kwenye mabanda yao, hivyo tumeona tugawane majukumu, baadhi yetu wako bandani kutoa elimu na huduma kwa watakaofika na sisi tunapita banda kwa banda kuwahudumia.” amefafanua Kumba, ambaye alifuatana na maafisa wengine wa Mfuko kwenye zoezi hilo.


Akifafanua, amesema kwa sasa karibu huduma zote za Mfuko zinapatikana kidijitali kupitia (PSSSF portal) ambapo kupitia simu janja au komphyuta, mwanachama anaweza kujihudumia yeye mwenyewe. Hivyo ni rahisi kuwapatia elimu kwenye mabanda yao ya jinsi ya kutumia huduma hiyo.
Kwa upande wao wanachama waliofikiwa na maafisa wa PSSSF, walifurahishwa na hatua hiyo kwani imewasaidia wale ambao walikuwa na changamoto na kuhitaji ufafanuzi kupata fursa ya kupata majawabu.

“Tumefurahi kutembelewa na PSSSF kutuletea huduma kwenye banda letu, ni kitu kizuri kwani mimi nimeweza kuunganishwa na PSSSF Kidijitali kwenye simu yangu,” amesema Mulegi Majogoro, mtumishi wa Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo.
Naye, Natalis Liduma, kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi, aliipongeza serikali kwa kuwezesha kusaidia ofisi kufanya kazi kwa kutumia mifumo.
“Mfumo wa PSSSF Kidijitali, umerahisisha na kuboresha utendaji kazi, ni mfumo rahisi na rafiki sana kwa mtumishi kuweza kupata taarifa zake kwa kutumia kiganja.” amesema Liduma.






