Dar es Salaam, Juni 16, 2026 – Benki ya EximTanzania leo imeingia katika ushirikiano wa kimkakati na kampuni ya Africarriers kwa lengo la kurahisha na kutoa dhamana nafuu za ununuzi wa magari kwa watu binafsi, wafanyabiashara, wamiliki wa biashara ndogo na za kati kote nchini.
Ushirikiano huu unadhihirisha dhamira ya dhati ya Benki ya Exim Tanzania ya kutoa zaidi ya huduma zakibenki kwa wananchi na kutoa suluhisho bunifu kwa wateja ili kukidhi mahitaji yao yanayobadilika kila siku na hatimaye kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.
Kupitia huduma hii ya ufadhili wa magari, wateja wapya na waliopo wa Benki ya Exim Tanzania watapata mikopo ya kununua magari mapya na yaliyotumika ya aina mbalimbali, ikiwemo chapa zinazozidi kupata umaarufu kutokana na ubunifu na ubora wake kama Jetour, Eicher, Sany na JAC Motors. Huduma hii inatoa masharti nafuu ya malipo ya awali pamoja na mpango mzuri na nafuu wa marejesho unaobadilika kulingana na uwezo wa mteja. Huduma hii inalenga kuwezesha umiliki wa magari kwa njia rahisi na ya gharama nafuu zaidi kwa watu binafsi, familia na wamiliki wa biashara mbalimbali.
Wateja watanufaika na malipo ya kila mwezi yenye unafuu kwa kipindi cha hadi miezi 72, jambo linalofanya ndoto ya kumiliki gari la kuaminika na lenye ubora wa hali ya juu kufikiwa kwa urahisi zaidi kuliko wakati mwingine wowote
Akizungumza wakati wa hafla ya kusaini makubaliano hayo, Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya Exim Tanzania Shani Kinswagaalisema ushirikiano huo umebuniwa mahsusi kwa ajili ya kuwahudumia makundi mbalimbali ya wateja, ikiwemo waajiriwa, wamiliki wa biashara, wajasiriamali, watu wenye kipato kikubwa, biashara ndogo na za kati pamoja na taasisi za kibiashara zinazohitaji suluhisho bora za usafiri bila kuathiri mtaji wao wa uendeshaji.
“Benki ya Exim Tanzania tunaendelea kujizatiti kwa kutumia ubunifu wa hali ya juu kuwawezesha wateja wetu na kuwasaidia kufikia malengo yao. Ushirikiano wetu na Africarriers unatuwezesha kutoa huduma rahisi na zinazobadilika za ufadhili wa magari ambazo zitawawezesha watu binafsi na wamiliki wa biashara kupata usafiri wa kuaminika huku wakihifadhi rasilimali zao za kifedha kwa mahitaji mengine muhimu,” alisema Shani.
Mpango wa Ufadhili wa Umiliki wa Magari kupitia Benki ya Exim unawapa fursa wateja wetu ya kupata magari mapya au yaliyotumika kwa urahisi zaidi. Wateja watahitajika kuchangia asilimia 20 hadi 30 tu ya gharama ya gari kama malipo ya awali, huku malipo kwa wauzaji wa magari yakifanywa moja kwa moja ili kuhakikisha mchakato wa ununuzi unakuwa rahisi na wa haraka zaidi. Kwa kurahisisha upatikanaji wa magari kwa wateja wetu, mpango huu unatarajiwa kuongeza tija, kuwezesha ukuaji wa biashara na kuchochea shughuli za kiuchumi nchini Tanzania. Aliongeza Shani.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Fedha wa Kundi la Africarriers, Mustafa Rashid, alisema kuwa kwa kuunganisha mpango mpana wa upatikanaji wa magari unaotolewa na Africarriers na uwezo wa Exim Bank katika utoaji wa huduma za mikopo na ufadhili, taasisi hizo mbili zimeleta suluhisho rahisi na yenye tija ya kuwawezesha watu binafsi na wafanyabiashara kumiliki magari.
“Ushirikiano huu ni udhihirisho wa dhati wa dhamira yetu ya kutoa suluhisho za usafiri zinazofikika na kuaminika kwa Watanzania. Kwa kushirikiana na Benki ya Exim Tanzania, tunawapa wateja chaguo bora na rahisi la kumiliki magari huku likichochea ukuaji wa biashara na maendeleo ya uchumi wa nchi,” alisema Mustafa.
Ushirikiano huu unaakisi dhamira ya pamoja ya taasisi hizi mbili katika kupanua upatikanaji magari na kuwawezesha Watanzania wengi zaidi kutimiza ndoto zao za kumiliki magari, ikiwemo magari mapya kabisa. Kupitia huduma hii, watu binafsi na familia wataweza kubadilisha ndoto zao kuwa uhalisia huku wakifurahia urahisi, uhuru na fursa mbalimbali zinazotokana na umiliki wa gari.
Exim Bank inawahimiza wateja wake kutembelea tawi lolote la benki hiyo au yadi za magari za Africarriers zilizopo kote nchini ili kupata taarifa zaidi kuhusu huduma hii na aina mbalimbali za magari yanayopatikana, na kisha kuchukua hatua kuelekea kumiliki magari bora ya ndoto zao.
Kuhusu Exim Bank Tanzania
Benki ya Exim Tanzania ilianzishwa mwaka 1997. Ni miongoni mwa taasisi za fedha zinazoongoza nchini, ikitambulika kwa ubunifu, utoaji wa huduma zinazomlenga mteja na mchango wake mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania. Benki hii ambayo inapatikana pia kikanda katika nchi za Comoro, Djibouti, Uganda na Ethiopia, ni miongoni mwa benki chache zilizoanzishwa Tanzania ambazo zimefanikiwa kupanua shughuli zake nje ya mipaka ya nchi. Kupitia mtandao wake mpana wa matawi na huduma za kisasa za kidijitali, Benki ya Exim Tanzania inaendelea kuwawezesha watu binafsi na biashara kupata huduma za kifedha zenye kuaminika, bunifu na ufanisi.
Kuhusu Africarriers Limited
Africarriers Limited ilianzishwa mwaka 1976 ikiwa ni yadi ndogo ya magari pamoja na gereji jijini Dar es Salaam. Leo hii imekua miongoni mwa Kampuni kubwa inayofanya biashara ya magari Afrika Mashariki na Kati. Kampuni hii ni sehemu ya Africarriers Group na inaongoza shughuli za biashara ya magari ya matumizi binafsi na ya kibiashara. Shughuli zake zimekuwa na mchango mkubwa katika kuendeleza sekta ya viwanda nchini Tanzania na kwa ukanda mzima.




