Bunge la Seneti la Marekani limetaka kuanza kwa mazungumzo ya maridhiano kati ya Serikali inayoongozwa na CCM na vyama vya upinzani, ikiwa ni sehemu ya mapitio ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya Marekani na Tanzania.
Sharti hilo limejumuishwa katika fasili B(4) ya kifungu cha saba cha Muswada wa Mapitio ya Uhusiano wa Uwili kati ya nchi hizo mbili uliowasilishwa Juni 17, 2026.
“Kuanza kwa mazungumzo na viongozi wa vyama vya upinzani kujadili kuhusu maridhiano hasa baada ya matukio ya vurugu wakati wa uchaguzi wa Oktoba 29, 2025,” kimeeleza kifungu hicho.
Hatua hiyo inaonekana kuendana na msimamo wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ambaye awali alieleza utayari wa kuanzisha mchakato wa maridhiano ya kitaifa na kutangaza mpango wa kuunda Tume ya Maridhiano kwa lengo la kuimarisha umoja na mshikamano wa Watanzania.
Hatua hii ya Marekani inaweza kupokewa vibaya na baadhi ya wanaharakati ambao kabla, wakati na baada ya vurugu za Oktoba 29, 2025 wamekuwa wakipinga kufanyika kwa maridhiano ya aina yoyote hapa nchini.





