Kanisa la ROC Dodoma limeendesha mafunzo ya ulinzi na usalama binafsi kwa watoto ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuwajengea uwezo wa kujilinda dhidi ya changamoto na vitisho mbalimbali vinavyowakabili katika jamii.
Mafunzo hayo yalilenga kuimarisha uelewa wa watoto kuhusu masuala ya usalama kuanzia ngazi ya familia hadi jamii, sambamba na kuwahamasisha kuwa makini katika kutambua viashiria vya hatari vinavyoweza kuhatarisha maisha yao.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mkuu wa Polisi Jamii wa Wilaya ya Kipolisi Mtumba, Mrakibu wa Polisi (ASP) Charles Mwamtobe, aliwataka watoto kuwa waangalifu na kutambua mapema vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama wao, ikiwemo ukatili, unyanyasaji wa kijinsia, matumizi mabaya ya teknolojia, dawa za kulevya, biashara haramu ya binadamu na ushawishi wa makundi yenye mienendo isiyofaa.
Alisisitiza kuwa mtoto ni rasilimali muhimu kwa familia, jamii na taifa, hivyo anapaswa kulindwa na kupewa malezi bora yatakayomwezesha kukua katika mazingira salama yenye maadili mema.
“Ulinzi na usalama wa mtoto si jukumu la serikali au wazazi pekee, bali ni wajibu wa kila mwanajamii kuhakikisha watoto wanapata mazingira salama ya kukua na kutimiza ndoto zao,” alisema ASP Mwamtobe.




Washiriki wa mafunzo hayo pia walihimizwa kutoa taarifa kwa wazazi, walezi, viongozi wa dini au vyombo vya dola wanapokumbana na vitendo vinavyohatarisha usalama wao au wa wenzao.
Aidha, mafunzo yaligusia matumizi salama ya mitandao ya kijamii na teknolojia ya mawasiliano, yakisisitiza umuhimu wa kujikinga dhidi ya ulaghai, unyanyasaji wa mtandaoni na athari nyingine zinazoweza kujitokeza kutokana na matumizi yasiyo sahihi ya teknolojia.
Kwa upande wake, Kanisa la ROC Dodoma limesema linaendelea kutumia kambi zake za watoto kama jukwaa la kuwajenga washiriki kiroho, kimwili na kijamii kupitia elimu mbalimbali zinazolenga kuwaandaa kuwa raia wema na viongozi bora wa baadaye.
Kanisa hilo pia liliwakumbusha washiriki mafundisho ya Mithali 22:6 yanayohimiza malezi bora ya mtoto ili akue katika njia njema na kuwa na mchango chanya kwa jamii.








