RUFIJI, PWANI: Serikali imesema imejipanga kupata suluhisho la kudumu la migogoro kati ya wakulima na wafugaji kwa kuimarisha mipango ya matumizi bora ya ardhi na kuhamasisha ufugaji wa kisasa, hatua inayolenga kuimarisha usalama wa chakula na kukuza uchumi wa Taifa.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Balozi Dk. Bashiru Kakurwa, Julai 20, 2026, wakati wa ziara ya kikazi wilayani Rufiji, ambapo alitembelea wafugaji na wakulima wa Kijiji cha Chumbi, kukagua maendeleo ya mpango wa Ranchi Ndogo na Vitalu vya Kilimo vya Kijiji cha Nyamwage, kabla ya kufanya mkutano wa hadhara katika Tarafa ya Ikwiriri.
Dk. Kakurwa alisema wakulima na wafugaji ni mhimili muhimu wa uchumi na usalama wa chakula, hivyo migogoro inayowakabili lazima ipatiwe ufumbuzi wa kudumu kupitia usimamizi mzuri wa matumizi ya ardhi.

“Bila wakulima na wafugaji Taifa haliwezi kuwa na usalama wa chakula. Kadri idadi ya watu inavyoongezeka, ndivyo mahitaji ya ardhi yanavyoongezeka. Suluhisho ni kupanga matumizi ya ardhi na kuhakikisha kila mmoja anaheshimu maeneo yaliyotengwa kwa shughuli zake,” alisema.
Alibainisha kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais–TAMISEMI pamoja na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi itapeleka timu za wataalamu katika maeneo yenye migogoro ili kuboresha mipango ya matumizi ya ardhi na kurekebisha changamoto zilizopo.
Waziri huyo pia aliwahimiza wafugaji kuachana na utegemezi wa malisho ya asili pekee kwa kuanza kuzalisha, kuvuna na kuhifadhi malisho kwa ajili ya matumizi ya kipindi cha kiangazi.


“Mfugaji wa kisasa anatakiwa azalishe malisho yake kama mkulima anavyozalisha chakula chake. Serikali ipo tayari kuwasaidia wafugaji kuongeza tija kupitia mfumo huu,” alisisitiza.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Luteni Kanali Frederick Komba, alisema tangu mwaka 2023 wilaya hiyo imeanzisha vitalu 371 vya Ranchi Ndogo, ambapo 334 tayari vimegawiwa wafugaji na baadhi yao wameanza kuvitumia.
Alikiri kuwa bado kuna changamoto ya baadhi ya wafugaji kusita kuachana na mfumo wa ufugaji wa kuhamahama, lakini elimu inayoendelea kutolewa imeongeza mwitikio wa kuhamia mfumo wa ufugaji wa kisasa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Rufiji, Rajabu Mbonde, alisema amani kati ya wakulima na wafugaji ni msingi wa maendeleo ya wilaya hiyo, akisisitiza umuhimu wa kuheshimu matumizi yaliyopangwa ya ardhi.


“Tunahitaji nyama, maziwa na chakula. Hatuwezi kukubali migogoro iendelee. Ng’ombe wabaki kwenye maeneo ya ranchi na wakulima walime katika maeneo yaliyotengwa kwa shughuli hiyo,” alisema.
Ziara ya Waziri ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuimarisha matumizi bora ya ardhi, kuendeleza mfumo wa Ranchi Ndogo na kuhakikisha migogoro kati ya wakulima na wafugaji inapungua kwa manufaa ya uzalishaji, usalama wa chakula na maendeleo ya uchumi wa Taifa.






