HomeGeneral NewsTVLA yaonya matumizi ya dawa bila vipimo vya mifugo 

TVLA yaonya matumizi ya dawa bila vipimo vya mifugo 

Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) imewahimiza wafugaji nchini kupeleka sampuli za mifugo katika vituo vyake vya kanda kwa ajili ya uchunguzi wa magonjwa kabla ya kutumia dawa, ili kubaini chanzo halisi cha ugonjwa na kuhakikisha mifugo inapatiwa tiba sahihi.

Rai hiyo imetolewa Agosti 7, 2026 na Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti na Maendeleo ya Teknolojia wa TVLA, Dk. Jelly Chang’a, alipokuwa akitoa elimu kwa wafugaji na wadau wa sekta ya mifugo waliotembelea banda la TVLA katika Maonesho ya Kilimo ya NaneNane 2026 yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. John Malecela, Nzuguni, jijini Dodoma.

Dk. Chang’a amesema uchunguzi wa maabara ni muhimu katika kufanya maamuzi sahihi ya matibabu kwa kuwa husaidia kubaini aina ya ugonjwa unaoathiri mifugo kabla ya kuanza matumizi ya dawa.

Amesema hatua hiyo husaidia kupunguza matumizi yasiyo sahihi ya dawa, kuongeza ufanisi wa matibabu na kuzuia wafugaji kutumia dawa ambazo huenda zisilingane na ugonjwa unaosumbua mifugo yao.

“TVLA ina mtandao wa maabara na vituo vya kanda vinavyotoa huduma za uchunguzi wa magonjwa ya mifugo. Tunawahimiza wafugaji kutumia huduma hizi kwa kupeleka sampuli za mifugo yao mapema ili wataalamu waweze kufanya uchunguzi na kutoa majibu yatakayowezesha mifugo kupata tiba stahiki,” amesema Dk. Chang’a.

Aidha, amewataka wafugaji kuzingatia ratiba za chanjo kwa kufuata kalenda zinazopendekezwa na wataalamu wa mifugo, akisisitiza kuwa kinga ni njia bora na yenye gharama nafuu ya kudhibiti magonjwa ya mifugo kuliko kusubiri mifugo iugue ndipo ianze kutibiwa.

Kwa mujibu wa Dkt. Chang’a, TVLA inaendelea kuzalisha chanjo mbalimbali kwa ajili ya mifugo na kuku, sambamba na kutoa huduma za uchunguzi wa magonjwa, uchunguzi wa ubora na usalama wa vyakula vya mifugo pamoja na huduma nyingine za maabara.

Amesema huduma hizo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha afya ya mifugo, kuongeza uzalishaji na kulinda afya ya jamii.

Kwa upande wao, baadhi ya wafugaji na wadau waliotembelea banda la TVLA wamesema elimu waliyoipata imewasaidia kuelewa umuhimu wa kufanya uchunguzi wa magonjwa kabla ya kutumia dawa, pamoja na kuzingatia matumizi sahihi ya chanjo.

Wameahidi kutumia huduma zinazotolewa na TVLA ili kuboresha afya na kuongeza uzalishaji wa mifugo yao.

Kupitia ushiriki wake katika Maonesho ya Kilimo ya NaneNane 2026, TVLA inaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu huduma zake mbalimbali, zikiwemo uchunguzi wa magonjwa ya mifugo, uzalishaji wa chanjo, uchunguzi wa ubora wa vyakula vya mifugo, usajili na uhakiki wa viuatilifu vya mifugo pamoja na huduma nyingine za maabara.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments