Uongozi wa Azam FC umesema ushiriki wao katika michuano maalum ya maandalizi inayoendelea Rwanda ni kwa ajili ya kumpa kocha Florent Ibenge nafasi ya kukijenga kikosi, na siyo kushinda kombe.

Mkuu wa Idara ya Habari wa Azam, Thabit Zacharia ‘Zaka’, alisema michuano hiyo ya APR Pre Season itawasaidia kupata mechi nyingi za kirafiki, kuona uimara na mapungufu ya timu kabla ya kuanza Ligi Kuu na mashindano ya kimataifa, ikiwemo Kombe la Shirikisho Afrika.
“Hatuchezi kwa ajili ya kombe, ila kama tukishinda ni sawa. Lengo letu ni kumpa kocha nafasi ya kujaribu mifumo na kutambua mapungufu kabla ya msimu kuanza,” alisema Zaka.
Michuano hiyo inashirikisha Azam, Power Dynamos (Zambia), Polisi FC, AS Kigali na wenyeji APR. Azam imepangwa kuanza hatua ya awali ya Kombe la Shirikisho kwa kucheza dhidi ya El Merreikh ya Sudan.




