Watanzania wametakiwa kuondoa dhana kwamba gofu ni mchezo wa matajiri pekee, bali ni wa watu wa rika zote, huku wazazi na walezi wakisihiwa kuwaruhusu watoto wao, hususan wa kike, kujifunza.

Wito huo umetolewa na Meja Jenerali Wilbert Ibuge kwenye mashindano ya “Maisha ni Hesabu” yaliyofanyika Klabu ya Gofu Lugalo, Dar es Salaam.
Mashindano hayo yalihusisha wachezaji mbalimbali na washindi wake wataiwakilisha nchi katika mashindano ya Afrika Mashariki, Novemba mwaka huu jijini Nairobi.
Aidha, wachezaji walioshinda akiwemo Nsajigwa Mwansasu na Vicky Elias waliwataka Watanzania kujiunga na mchezo huo wakisisitiza si mchezo wa matajiri pekee, bali ni fursa ya kujifunza, kupata ujuzi na hata ajira. Waandaaji walisema maandalizi mazuri kwa vijana yanaweza kuifanya Tanzania kufanikisha uwakilishi bora kimataifa.




