Mkuu wa Wilaya ya Handeni mkoani Tanga, Salum Nyamwese, amekemea tabia ya baadhi ya waendesha bodaboda kufanya vitendo vya kihatarishi barabarani ikiwemo kunyanyua mguu mmoja maarufu kama vishwandu, akisema ni hatari kwa maisha yao na abiria wanaowabeba.

Akizungumza na waendesha bodaboda na bajaji katika mkutano uliofanyika Uwanja wa Shule ya Msingi Chanika, mjini Handeni, Nyamwese amesisitiza umuhimu wa kufuata sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali.
Wito wa Kuchangamkia Mikopo Isiyo na Riba
Katika mkutano huo, DC Nyamwese aliwataka waendesha bodaboda na bajaji kuchangamkia fursa ya mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri ya Mji Handeni kupitia mapato ya ndani, akieleza kuwa mikopo hiyo haina riba na itawawezesha kumiliki vyombo vya usafiri badala ya kuendelea kuteseka na mikataba kandamizi.
“Dhamira ya Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni kuhakikisha Watanzania wanapata maendeleo, ikiwemo ninyi maafisa usafirishaji. Hivyo mnapaswa kuchangamkia fursa zilizopo ili mjikwamue kiuchumi,” amesema Nyamwese.

Mafunzo ya Bure ya Kuongeza Ujuzi
Pia, DC huyo amebainisha kuwa serikali ya wilaya imeandaa mpango wa mafunzo ya bure ya wiki moja kupitia Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Handeni, yatakayowawezesha waendesha bodaboda kupata vyeti vitakavyorahisisha mchakato wa kuomba leseni rasmi.
Maombi ya Umoja wa Bodaboda Handeni
Awali, akisoma risala ya Umoja wa Bodaboda Handeni, Hamis Kidunda alisema umoja huo wenye wanachama 1,265 unaomba serikali kuendelea kuwawezesha kupata mikopo ya pikipiki na bajaji ili kuondokana na mikopo kandamizi.





