Sunday, December 7, 2025
spot_img
HomeHabariDk. Jingu: Mafunzo ya wanawake yakuza viongozi wenye maadili na uwezo

Dk. Jingu: Mafunzo ya wanawake yakuza viongozi wenye maadili na uwezo

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. John Jingu, amesema kuwa mafunzo ya wanawake katika uongozi yanalenga kuwajengea uwezo Ili wawe viongozi wazuri na wenye kuleta mabadiliko na maendeleo.

Dk. Jingu ameyasema hayo jijini Dar es Salaam wakati akifungua kongamano la tano la Wanawake katika Uongozi lililoandaliwa na Taasisi ya Uongozi chini ya dhima ya ‘Mchango wa wanawake katika uongozi barani Afrika’.

Amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wanawake ili wawe viongozi wazuri na mchango wa maendeleo katika maeneo waliyopo.

“Viongozi wanatengenezwa hivyo Taasisi ya Uongozi inaendeleza adhima hiyo kwa kutoa mafunzo ili kupata wanawake watakaoshika nafasi za juu za uongozi si kwa sababu za kijinsia bali kutokana na uwezo na sifa walizonazo,” amesema Dk. Jingu.

“Msingi wa hayo yote ni kwamba viongozi wazuri wanatengenezwa baadhi wanaweza kuzaliwa na vipaji mbalimbali na uwezo wa kiuongozi, wakitengenezwa na kujengewa sifa zinazohitajika wanaweza kutoa mchango mzuri zaidi wa maendeleo katika maeneo au sekta walizopo,”.

Dk. Jingu Amesema maafunzo hayo ya uongozi ni mazuri kwa sababu yanatoa fursa kwa wanawake kubadilishana uzoefu wao na watu waliopo kwenye nafasi za uongozi, kila mshiriki katika mafunzo haya ana kocha wake ambaye anamlea na kumsaidia.

Aidha, amesema kongamano hilo, ambalo limekuwa jukwaa muhimu katika kukuza uongozi wa wanawake barani Afrika, limewakutanisha washiriki kutoka serikalini, sekta binafsi, vyuo vikuu, na asasi za kiraia.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Uongozi, Kadari Singo, amesema programu mpya ya Wanawake katika Uongozi imelenga kuwajengea uwezo wanawake ili wanapochukua nafasi za kiuongozi kuzitumia vyema na hatimaye kuongeza uwakilishi wa wanawake katika nafasi za juu za kisiasa, kiuchumi na kibiashara.

Singo amesema takwimu zinaonesha kwamba mpaka sasa kuna asilimia 33 pekee ya wanawake wanaoshikilia nafasi kubwa za maamuzi duniani, hivyo kufika uwiano wa 50 Kwa 50 inahitajika jitihada hizo.

“Taasisi ya Uongozi imekuwa ikifanya jitihada kuhakikisha kwamba wanaendelea kuwajengea uwezo ili kupata wanawake wengi wenye sifa za kushikilia nafasi za uongozi barani Afrika ikiwemo Tanzania,” amesema

“Mwitikio wa wanawake kushiriki mafunzo haya umekuwa mkubwa, miaka ya nyuma tunapotangaza kuanza kwa kodi waliokuwa wanaomba walikuwa kati ya 500 hadi 600, mwaka huu walioomba viongozi kutoka barani Afrika ni 2009 waliopata ni 100, kati ya watu hao walioomba wanatoka Botswana, Namibia, Cameroon, Kenya, Uganda, Marekani, Uingereza na Sweden,”

Aidha Singo amesema wamefanya utafiti mdogo na kubaini kuwa wanawake wengi waliopata mafunzo kwao wameongeza uelewa katika masuala ya uongozi, wameendelea kujiamini na kupata mbinu mpya za ufanyaji wa kazi katika maeneo yao.

Ofisa Mipango wa Umoja wa Ulaya, Alessandro Pisani, alisema kongamano hilo limepiga hatua katika juhudi za pamoja za kuweka usawa wa kijinsia kama kipaumbele katika ajenda ya maendeleo ya Afrika.

Alisisitiza ushirikiano wa Umoja wa Ulaya, Serikali ya Tanzania, na UN Women katika kuvunja vikwazo vya kimfumo vinavyozuia uongozi wa wanawake.

Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya Usawa wa Kijinsia (UN Women), Katherine Gifford, alisema mpango huo wa utoaji mafunzo kwa wanawake ni hitaji la kimaendeleo linalopaswa kutoa matokeo zaidi ya uwakilishi pekee.

“Tunahitaji mifumo endelevu ya kusaidia wanawake kufika katika ngazi za maamuzi,” alisema Gifford.

Naye Balozi wa Finland nchini Tanzania, Theresa Sitting, Amesema uongozi siyo cheo bali ni kujitambua na kuwa na uvumilivu unapokabiliwa na changamoto hivyo amewataka wanawake wasihofu kuanguka wakipatwa na hali hiyo au kukosa walichotamani wanapaswa kusimama tena na kujaribu upya.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments