Sunday, December 7, 2025
spot_img
HomeHabariTVLA yaendelea kusikiliza wateja kupitia Wiki ya Huduma kwa Wateja

TVLA yaendelea kusikiliza wateja kupitia Wiki ya Huduma kwa Wateja

Dodoma, Oktoba 2025 — Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) imeendelea kusogeza huduma karibu na wateja wake kwa kuwatembelea wauzaji wa bidhaa zake katika mikoa ya Iringa na Dodoma, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja yanayofanyika kitaifa kuanzia Oktoba 6 hadi 11, 2025.

Ziara hizo zilizofanyika Oktoba 9 na 10, 2025, ziliongozwa na Afisa Masoko wa TVLA, Fihiri Mbawala, ambaye alitembelea maduka mbalimbali yanayouza bidhaa za TVLA — hususan chanjo za mifugo — kwa lengo la kusikiliza maoni ya wateja, kujadili changamoto na kuangalia mbinu za kuboresha huduma.

“Tunatambua mafanikio ya TVLA yanategemea kuridhika kwa wateja wetu. Ndiyo maana tumeamua kutoka ofisini na kuwafuata moja kwa moja ili kusikia kutoka kwao nini kifanyike kuboresha huduma,” alisema Bw. Mbawala.

Aliongeza kuwa TVLA itaendelea kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa bora na salama zinazokidhi viwango vya kitaifa na kimataifa, huku akisisitiza umuhimu wa mawasiliano endelevu kati ya taasisi hiyo na wauzaji wa bidhaa zake.

Kwa upande wao, wauzaji wa bidhaa za TVLA wamepongeza hatua hiyo. Zainabu Mdegela kutoka mkoani Iringa alisema TVLA imeonyesha dhamira ya dhati ya kuwajali wateja kwa kuwafikia moja kwa moja madukani, jambo linalowapa nafasi ya kueleza changamoto na kutoa ushauri.

Naye John Mushi wa Dodoma alishauri taasisi hiyo kuimarisha mawasiliano ya taarifa za bidhaa na bei kupitia mifumo ya kidijitali, pamoja na kutoa mafunzo kuhusu utunzaji sahihi wa chanjo.

Wiki ya Huduma kwa Wateja huadhimishwa kila mwaka duniani kote, ikilenga kutambua mchango wa wateja na kuhimiza taasisi mbalimbali kuboresha ubora wa huduma. TVLA imekuwa miongoni mwa taasisi za Serikali zinazotumia wiki hiyo kujenga uhusiano wa karibu na wadau wa sekta ya mifugo nchini.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments