Sunday, November 9, 2025
spot_img
HomeHabariWizara sita zakutana kujadili kasi ya utekelezaji wa mradi wa Bwawa la...

Wizara sita zakutana kujadili kasi ya utekelezaji wa mradi wa Bwawa la Kidunda

Viongozi kutoka taasisi na wizara sita za Serikali wamekutana mkoani Morogoro kujadili hatua za pamoja katika utekelezaji wa mradi mkubwa wa bwawa la maji la Kidunda, ikiwa ni juhudi za kuhakikisha mradi huo wa kimkakati unakamilika kwa wakati na kwa ufanisi.

Kikao hicho kimehusisha Wizara ya Maji, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Fedha, Wizara ya Nishati, Tume ya Mipango na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.

Mradi wa bwawa la Kidunda unatekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 329 na unatarajiwa kunufaisha mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro kwa kuongeza upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi.

Akiongoza kikao kazi hicho, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, alisema ushirikiano wa wizara na taasisi mbalimbali ni muhimu katika kuhakikisha mradi huo unaotekelezwa kwa fedha za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unafikia malengo yake.

“Tumekutana na wizara muhimu za kisekta zinazochangia ukamilishaji wa mradi wa Kidunda ili kubaini maendeleo yaliyofikiwa, sambamba na kutatua changamoto zilizopo. Ushirikiano wa kisekta ni muhimu sana kwani kwa pamoja tutasaidiana kuja na mipango bora zaidi ya utekelezaji wa mradi huu muhimu kwa wananchi,” alisema Mhandisi Mwajuma.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu utunzaji wa mazingira na ulinzi wa vyanzo vya maji, ili kuepuka uharibifu utakaoweza kuathiri ujazo wa bwawa pindi litakapokamilika.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Musa Ali Musa, alitoa wito kwa watekelezaji wa mradi huo kuhakikisha wanafanya kazi kwa karibu na wananchi wa maeneo yanayozunguka bwawa hilo.

“Ni muhimu wananchi wakahusishwa ipasavyo ili kuepuka malalamiko ambayo yanaweza kuchelewesha au kuleta changamoto katika utekelezaji wa mradi huu wa kimkakati,” alisema Dkt. Musa.

Mradi wa Bwawa la Kidunda ni miongoni mwa miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali kwa lengo la kuboresha huduma ya maji, kukuza uchumi wa viwanda, na kulinda rasilimali za maji nchini.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments