Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu, amesisitiza kuwa kinga ya jamii ni nguzo muhimu ya ustawi wa wafanyakazi na kwamba waajiri wanapaswa kuendelea kutekeleza wajibu wao kwa kuhakikisha michango yote ya kisheria inawasilishwa kwa wakati.
Amesema uchumi imara hujengwa na waajiri wanaotekeleza wajibu wao kwa uaminifu, huku akieleza kuwa michango ya wafanyakazi ni dhamana ya maisha bora ya sasa na ya baadaye. Aidha, ametoa wito wa ushirikiano katika kujenga Tanzania yenye kazi zenye staha na mazingira bora ya ajira.
Sangu amebainisha kuwa mahusiano mazuri ya kikazi huanza kwa kuheshimu sheria, na kwamba kuwasilisha michango kwa wakati ni ishara ya uwajibikaji na njia ya kulinda haki za wafanyakazi pamoja na kuimarisha ustawi wa sekta ya kazi nchini.
Ameongeza kuwa michango ya wafanyakazi si gharama kwa waajiri, bali ni uwekezaji katika rasilimali watu na maendeleo ya Taifa, akihimiza kujengwa kwa utamaduni wa kuwasilisha michango kwa wakati ili kuimarisha uchumi na kazi zenye staha.






Kauli hiyo imetolewa sambamba na Mkutano Mkuu wa 67 wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), uchaguzi wa viongozi na kongamano la waajiri lililofanyika jijini Dar es Salaam, leo Juni 25,2026 ambapo Mwenyekiti wa ATE, Oscar Mgaya, ametoa hotuba fupi ya ufunguzi.
Katika kongamano hilo, Mkuu wa Kitengo cha Utafiti, Sera na Utetezi wa ATE, Renatus Mbamilo, amesema uchumi endelevu unategemea uwiano mzuri kati ya kinga ya jamii na uendelevu wa biashara. Alieleza kuwa ushirikiano wa kimkakati kati ya waajiri, wafanyakazi na taasisi mbalimbali, pamoja na mifumo bora ya udhibiti, unawanufaisha wadau wote.
Mbamilo pia amewasilisha mada kuhusu umuhimu wa kuimarisha kinga ya jamii na uendelevu wa biashara kupitia ushirikiano wa kimkakati, ufanisi wa mifumo ya kisheria na ushirikiano wa taasisi.
Katika hatua nyingine, ATE na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) zilisaini hati ya makubaliano (MoU) yenye lengo la kuimarisha ushirikiano wa taasisi hizo na kukuza maeneo yenye maslahi ya pamoja. Makubaliano hayo yalisainiwa na Mtendaji Mkuu wa ATE, Wakili Suzanne Ndomba-Doran, pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba.






Kupitia ushirikiano huo, taasisi hizo zitakuza kubadilishana maarifa, kutekeleza miradi ya pamoja, kujenga uwezo wa watumishi na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi, huku zikichangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya Tanzania.
Mshomba amesema makubaliano hayo yataimarisha uzingatiaji wa sheria na kanuni pamoja na kutoa jukwaa la kushughulikia changamoto za pamoja kwa ufanisi zaidi. Pia yatawezesha utoaji wa huduma zilizo wazi, zenye ufanisi na zinazomlenga mwananchi.
Ameongeza kuwa ushirikiano huo utapanua elimu kwa umma kuhusu hifadhi ya jamii ili kuongeza uelewa wa waajiri na wafanyakazi kuhusu haki, wajibu na manufaa ya kinga ya jamii. Aidha, utawezesha mifumo ya taasisi hizo kuunganishwa kwa ajili ya kuboresha ubadilishanaji wa taarifa na kupunguza urudufu wa kazi.
Katika mkutano huo pia, Mtaalamu wa Ajira kutoka Shirika la Kazi Duniani (ILO), Annamarie Kiaga, amesisitiza umuhimu wa kukuza ajira zenye staha, kuongeza uzalishaji, kuendeleza ujuzi na kuimarisha majadiliano ya kijamii kama nguzo za ukuaji wa uchumi shirikishi na endelevu.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa TUCTA, Hery Mkunda, ameeleza umuhimu wa ushirikiano kati ya waajiri, wafanyakazi na wadau wa kijamii katika kuendeleza mazingira bora ya kazi, kuongeza tija na kukuza uchumi wa Taifa.






Mtendaji Mkuu wa ATE, Wakili Suzanne Ndomba-Doran, amesema mafanikio ya mkutano huo yametokana na ushirikiano, kuaminiana na kujitolea kwa wadau mbalimbali. Alisisitiza kuwa ATE itaendelea kushirikiana na Serikali, wafanyakazi na taasisi za hifadhi ya jamii ili kuunda ajira zenye staha, maeneo yenye tija ya kazi na uchumi endelevu.
Ameongeza kuwa ushirikiano kati ya ATE na NSSF unaonyesha jinsi taasisi zinavyoweza kuboresha huduma, kuimarisha uzingatiaji wa sheria na kuongeza thamani kwa waajiri na wafanyakazi. Pia ameeleza kuwa kanuni bora, ushirikiano wa kimkakati na taasisi imara ni msingi wa biashara zenye ushindani na ukuaji wa uchumi jumuishi.
Katika uchaguzi uliofanyika wakati wa Mkutano Mkuu wa 67 wa ATE, Oscar Mgaya alichaguliwa tena kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya ATE huku Imelda Lutebinga akichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo kuanzia 2026 hadi 2029.
Uongozi huo mpya umepewa dhamana ya kuendelea kutetea maslahi ya waajiri, kuimarisha majadiliano ya kijamii na kukuza mazingira bora ya biashara nchini. Wajumbe wa mkutano huo pia walipitia taarifa za mwaka za chama pamoja na taarifa za fedha zilizokaguliwa kabla ya kuhitimisha mkutano na kongamano la waajiri.





