Bunge la Tanzania limemthibitisha Deogratius Ndejembi, kuwa Makamu wa Rais mteule kwa asilimia 100, akisema dhamana aliyopewa haitapimwa kwa ujana wake, bali utii kwa Rais Samia Suluhu Hassan na uadilifu kwa Watanzania.
Ndejembi, amethibitishwa na Bunge, kwa kupigiwa kura za ndiyo na wabunge wote 324 waliokuwepo bungeni, sawa na asilimia 100. Hakukuwa na kura ya hapana wala iliyoharibika.




Akizungumza baada ya kuthibitishwa bungeni jijini Dodoma leo, Agosti 28, 2026 Ndejembi, amesema ukubwa wa dhamana hiyo hautapimwa kwa ujana wake, bali kwa utii kwa Rais, uadilifu kwa Watanzania, kazi yoyote atakayotumwa kuitekeleza na mkuu wa nchi.
Ameeleza anakwenda kuwa Makamu wa Rais sio wa Wana CCM pekee, bali vyama vyote na Watanzania kwa ujumla kama ilivyo kwa Rais wa nchi.
“Nitajitahidi kwa unyeyekevu mkubwa sana, kumsaidia Rais kuwa kiungo kwa Watanzania wote. Kama vile mapenzi yake yatakavyotaka kwa sababu nafanya kazi chini ya Rais Samia Suluhu Hassan,” amesema Ndejembi.






