Watanzania 174 waliokuwa wakiishi katika Jimbo la KwaZulu-Natal nchini Afrika Kusini wameishukuru Serikali kwa kuwawezesha kurejea nchini baada ya kukumbwa na vitisho na madhila yaliyowafanya kuishi kwa hofu.
Watanzania hao wamewasili nchini kwa ndege ya Air Tanzania, baada ya kuiomba Serikali iwasaidie kurejea kufuatia kuzorota kwa hali ya usalama na vitendo vya baadhi ya wazawa dhidi ya wageni.
Akizungumza baada ya kuwasili nchini, Pascal Dagama, mkazi wa Kigoma, amesema walikumbana na vitisho vya kuuawa na kupewa muda mfupi wa kuondoka katika maeneo waliyokuwa wakiishi.
Amesema hali hiyo iliwalazimu baadhi yao kuhama mara kwa mara na wengine kukosa makazi ya kudumu kutokana na hofu ya kuvamiwa na kupoteza maisha.
Dagama ameishukuru Serikali kwa kuingilia kati na kuwawezesha kurejea Tanzania, akisema hatua hiyo imewapa nafuu baada ya kipindi cha kuishi kwa hofu na kutokuwa na uhakika wa usalama wao.




