HomeAfyaMajaribio ya kliniki kulenga kuharisha kwa watoto na usugu wa dawa

Majaribio ya kliniki kulenga kuharisha kwa watoto na usugu wa dawa


TANZANIA imezindua utafiti wa majaribio ya kliniki unaohusisha nchi mbalimbali, unaolenga kuchunguza iwapo matumizi ya probiotics yanaweza kuongeza ufanisi wa chanjo ya rotavirus, kupunguza maambukizi ya magonjwa ya kuhara kwa watoto na kusaidia kukabiliana na usugu wa vimelea dhidi ya dawa za antimicrobial (AMR).

Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa mkutano wa kuanza rasmi kwa mradi wa ProRota, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI (Afya), Profesa Tumaini Nagu, amesema utafiti huo umefanyika kwa wakati muafaka kutokana na magonjwa ya kuambukiza kuendelea kuathiri afya za watoto.

Amesema utafiti huo unaohusisha Tanzania, Malawi, Côte d’Ivoire na Norway, unalenga kuzalisha ushahidi wa kisayansi utakaosaidia kuboresha kinga na udhibiti wa magonjwa ya kuhara kwa watoto.

Amesema magonjwa ya kuhara yanaongeza matumizi ya huduma za afya pamoja na matumizi ya antibiotics, hali inayochangia uhusiano kati ya maambukizi ya utotoni na kuongezeka kwa tishio la usugu wa vimelea dhidi ya dawa za antimicrobial.

“Utafiti huu una uwezo wa kutoa ushahidi wenye athari za moja kwa moja katika afya ya watoto, sera za chanjo, matumizi sahihi ya dawa za antimicrobial na utoaji wa huduma za afya ya msingi,” amesema.

Profesa Nagu amesema Tanzania imepiga hatua katika kupunguza vifo vya watoto, ambapo kiwango cha vifo vya watoto walio chini ya miaka mitano kimeshuka kutoka 65 hadi 43 kwa kila vizazi hai 1,000. Hata hivyo, amesema kasi ya kupungua kwa vifo vya watoto wachanga bado ni ndogo.

Amesema ushahidi kutoka hospitalini unaonyesha kuwa sepsis kwa watoto wachanga inachangia asilimia 13.6 ya vifo vya watoto hao, huku maambukizi mengine ya watoto wachanga yakichangia asilimia 8.8.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa (NIMR), Profesa Said Aboud, amesema NIMR itaongoza sehemu ya mradi inayohusu maadili ya utafiti ili kuhakikisha usalama na ustawi wa watoto watakaoshiriki katika utafiti huo.

Amesema NIMR itashirikiana kwa karibu na wadau wote wa mradi kuhakikisha haki, usalama na ustawi wa washiriki vinapewa kipaumbele katika kila hatua ya utafiti.

Amesema taasisi hiyo pia itaratibu Bodi ya Ufuatiliaji wa Usalama wa Takwimu na Mshauri Huru wa Maadili, pamoja na kushiriki katika kuwahusisha wananchi na tafiti za utekelezaji.

Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Profesa Bruno Sunguya, amesema jaribio hilo linaonyesha umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika kukabiliana na changamoto changamano za afya.

Amesema MUHAS ina mikataba ya makubaliano zaidi ya 200 na taasisi mbalimbali duniani na inaendelea kujikita katika kuimarisha tafiti, ubunifu na ushirikiano wa kimataifa.

Mratibu wa Mradi wa ProRota, Dk. Sabrina Moyo, amesema watunga sera, wataalamu wa afya na watekelezaji wa programu watakuwa miongoni mwa watumiaji muhimu wa ushahidi utakaopatikana kupitia utafiti huo.

Amesema maoni na mrejesho wao utasaidia kuhakikisha utafiti huo unalenga mahitaji halisi na matokeo yake yanaweza kutafsiriwa katika sera na utekelezaji utakaoboresha afya za watoto.

Mtafiti Mkuu wa mradi huo, Profesa Joel Mnyahi, amesema utafiti utachunguza nafasi ya probiotics katika kuzuia magonjwa ya kuhara, kuelewa uwezekano wa watoto kuambukizwa rotavirus na kupunguza usugu wa vimelea dhidi ya dawa za antimicrobial.

Mradi huo unaoungwa mkono na European and Developing Countries Clinical Trials Partnership (EDCTP), unatarajiwa kuzalisha ushahidi utakaosaidia kuimarisha kinga dhidi ya maambukizi kwa watoto, kuongeza ufanisi wa chanjo na kuunga mkono juhudi za kukabiliana na usugu wa vimelea dhidi ya dawa za antimicrobial barani Afrika.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments