PWANI: Umoja na ushirikiano miongoni mwa walimu wa Shule ya Msingi Juhudi wilayani Mkuranga umechangia kuongezeka kwa ufaulu wa wanafunzi wa Darasa la Saba kutoka asilimia 78 hadi 99.
Akizungumza katika mahafali ya tano ya Darasa la Saba, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Makarius G. Kihawa, amesema walimu wamekuwa wakifanya kazi kwa pamoja kuhakikisha wanafunzi wanafikia matokeo bora.
Amesema shule hiyo yenye zaidi ya wanafunzi 2,000 imekuwa ikivutia wanafunzi kutoka maeneo mbalimbali ya Mkuranga na Dar es Salaam kutokana na kutoa elimu bora.
Hata hivyo, amesema shule inakabiliwa na upungufu wa vyumba vya madarasa 78 pamoja na ukosefu wa uzio, hali inayohitaji matofali takribani 600,000 kwa ajili ya ujenzi.

Kihawa amesema Serikali imeanza kuliona tatizo hilo na kuamua kujenga shule nyingine kutokana na ongezeko kubwa la wanafunzi, huku wahitimu 275 wakitarajiwa kufanya mtihani wa Darasa la Saba mwaka huu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Shule hiyo, Zaina Abdallah, ameishukuru Serikali na wadau, akiwemo waliowezesha ujenzi wa vyoo vya kisasa na uwanja wa michezo, huku akiomba ujenzi wa uzio ili kuimarisha usalama wa wanafunzi.
Katibu Mwenezi wa CCM Wilaya ya Mkuranga, Omary Kisato, aliyemwakilisha Mbunge wa Mkuranga, Abdallah Ullega, amesema mbunge huyo amechangia Sh milioni mbili kusaidia kukabiliana na changamoto za vifaa vya kujifunzia na kufundishia, kompyuta na TEHAMA.
Nao wazazi na wanafunzi wameiomba Serikali na wadau wa elimu kusaidia kuboresha miundombinu, kuongeza vifaa vya kujifunzia na kufundishia pamoja na kuhakikisha wanafunzi wanapata huduma ya chakula shuleni.






