Na Julieth Mkireri,Kibaha
Wanafunzi zaidi ya 800 wa Shule ya msingi Zogowale Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha wamepokea msaada wa unga kwa ajili ya chakula cha mchana pamoja na vifaa vya steshenari.
Msaada huo wa zaidi ya Milion 5 umetolewa na mwekezaji wa kiwanda cha karatasi cha Fortune kilichopo kata ya misugusugu ambaye mbali ya misaada hiyo pia ametoa pampu kwa ajili ya maji ya kisima kurahisisha upatikanaji wa maji shuleni hapo.
Awali wanafunzi hao wamekuwa wakipata chakula kwa michango ya wazazi na baada ya kupokea mifuko hiyo 50 upo uwezekano wa msaada huo kuwa endelevu kwa shule hiyo utakaokuwa unatolewa na mwekezaji huyo.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo Meneja biashara wa kiwanda hicho Colin Yang amesema uwekezaji si tu ajira na kulipa kodi basi ni pamoja nakushirikiana na jamii.
“Tumesaidia chakula kwa wanafunzi na tutaona namna ya msaada huu kuwa endelevu tunachotaka kwa jamii isituone sisi kama wawekezaji tu bali wanajamii mwenzao tukishirikiana kwa mambo mengi kutatua changamoto,”amesema

Yang pia amesema mbali ya msaada huo pia wananchi zaidi ya 100 katika kata zinazoishi karibu na kiwanda cha cha karatasi wamewasogezea huduma ya maji karibu kuondoa changamoto walioyokuwa nayo awali.
Mkuu wa wilaya ya Kibaha Nickson John amesema kilichofanywa na mwekezaji huyo kinamuweka karibu na wananchi kuwa na mahusiano mazuri.
Nickson amesema kutolewa kwa msaada wa chakula haiwafanyi wazazi kuacha kuchangia chakula badala yake wakae na kamati ya shule na kuangalia utaratibu mzuri wakuwezesha wanafunzi hao kupata chakula cha kutosha.
Mwenyekiti wa Saeni Edward Kitale alisema katika eneo lake wawekezaklji hao ndio wakwanza kusaidia msaada wa chakula kwa wanafunzi na pampu shuleni kurahisisha upatikanaji wa maji.
Kitale amesema pia wawekezaji hao waliahidi kutengeneza barabara ya kuelekea shuleni kwa kuifanyia ukrabati ipitike wakati wote.
Mwanafunzi wa darasa la sita katika shule hiyo Irene Didas ameshukuru kwa msaada huo huku akiomba wadau wengine kusaidia upatikanaji wa mashine ya kutolea kopi mitihani





