Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwaw mgeni rasmi kwenue utoaji wa Tuzo za 19 za Rais kwa Wazalishaji Bora wa mwaka (PMAYA) zinazotarajiwa kufanyika kesho Jumatano.
Mkurugenzi wa Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI), Leodegar Tenga alisema jana kuwa madhumuni ya Tuzo hizo ni kutambua, kuthamini na kuenzi umuhimu na mchango wa sekta ya Viwanda katika kukuza Uchumi wa nchi, pamoja na kutoa fursa kwa wanachama wa CTI na wadau wake.
Alisema madhumuni mengine ni kukutana, kuzungumza na kubadilishana uzoefu katika kuendeleza sekta ya viwanda na uchumi kwa ujumla.
Aidha, alisema tuzo hizo hutumika kuhamasisha kuongeza uzalishaji na ushindani katika Sekta ya Viwanda na kwamba zilianzishwa rasmi mwaka 2005 na zimekuwa zikitolewa kila mwaka.
“Washindi wa Tuzo za Rais hupatikana kwa kuzingatia vigezo kadhaa. Vigezo muhimu ni pamoja na ufanisi katika uzalishaji, mauzo ya nje na kupata fedha za kigeni, uwekezaji katika teknolojia ya kisasa, matumizi bora ya nishati, utunzaji wa mazingira, afya na usalama wa wafanyakazi, uwiano wa kijinsia katika uongozi, pamoja na mchango katika jamii,” alisema

Alisema kutokana na mwelekeo wa dunia kuelekea maendeleo endelevu na uzalishaji unaozingatia hifadhi ya mazingira, toleo la mwaka huu limebeba kaulimbiu isemayo “Green Elegance – Celebrating Sustainable Manufacturing Practices.”
“Kaulimbiu hii inaakisi dhamira ya pamoja ya kujenga sekta ya viwanda inayokuza uchumi kwa njia endelevu, inayozingatia matumizi bora ya rasilimali, uzalishaji unaowajibika na utunzaji wa mazingira,” alisema.
Aidha,Tenga alisema kauli mbiu hiyo inaendana na jitihada za Serikali za kuharakisha maendeleo ya uchumi wa viwanda kupitia matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira, kuongeza ufanisi wa uzalishaji na kuunga mkono ajenda za kitaifa na kimataifa kuhusu kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, uchumi mzunguko (circular economy) na mageuzi ya kuelekea uchumi wa kijani.
“Ni muhimu kwa sekta za uzalishaji kuzingatia mbinu/kanuni mbalimbali za uzalishaji endelevu kwenye Mazingira, Kijamii na Utawala Bora (Environmental, Social and Governance (ESG). Hivi sasa uzalishaji kwa kuzingatia ESG umekuwa ni swala muhimu katika upatikanaji wa fedha, uwekezaji, ufikiaji wa masoko, kuongeza mnyororo ya thamani ya kimataifa na ushirikiano wa kibiashara,” alisema.


Alisema kwa kutambua umuhimu huu, CTI, kupitia Mkataba wa Ushirikiano wa Kimkakati na DANIDA kupitia Denish Industries (DI) iliendesha mafunzo ya kukuza uelewa wa ESG katika mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Arusha na Mwanza, na kufikia zaidi ya wanachama 200 wa CTI na wafanyabiashara wadogo na wa kati.
Aidha, Tenga alisema katika Tuzo za Rais za 19 za Mzalishaji Bora wa Mwaka (PMAYA), CTI imechagua Mabalozi 10 wa ESG na watatunukiwa vyeti na mabalozi hao watafuatiliwa na kutathminiwa kwa kipindi cha mwaka mzima kwa kuzingatia utekelezaji na matokeo ya ESG katika kampuni zao.
“Tathmini hiyo itatumika kumtambua kama ESG Champion atakayezawadiwa katika Tuzo za 20 za PMAYA ijayo na uteuzi na tathmini utazingatia, miongoni mwa mambo mengine, utekelezaji wa ESG kwa vitendo, matokeo yanayopimika katika maeneo ya mazingira, kijamii na utawala bora, uwajibikaji wa wafanyakazi katika kila ngazi, mchango katika kuendeleza jamii inayomzunguka, afya na usalama wa mazingira ya kazi,” alisema






