HomeHabariBaada ya malalamiko, AUWSA yarejesha huduma ya maji Matevesi

Baada ya malalamiko, AUWSA yarejesha huduma ya maji Matevesi

Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mjini, Joseph Mkude, amefanya ziara katika Kata ya Matevesi, Wilaya ya Arumeru, Mkoa wa Arusha, kwa lengo la kukagua hali ya upatikanaji wa huduma ya maji na kusikiliza changamoto zinazowakabili wananchi.‎‎

Katika ziara hiyo, Mkude ametembelea maeneo mbalimbali pamoja na baadhi ya nyumba za wananchi ili kujionea hali ya huduma ya maji na kupata mrejesho kuhusu upatikanaji wa huduma hiyo.‎‎

Amesema Serikali inaendelea kuweka mkazo katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma muhimu kwa uhakika, huku akipongeza jitihada zinazofanywa na Mamlaka ya Maji Arusha (AUWSA) katika kushughulikia changamoto za huduma ya maji katika maeneo mbalimbali.‎‎

Mkude amesema baadhi ya changamoto zilizokuwa zikikwamisha upatikanaji wa maji, ikiwemo changamoto za miundombinu na mabomba yanayofikisha maji kwa wananchi, zinaendelea kushughulikiwa ili kuhakikisha huduma hiyo inakuwa ya uhakika.

‎‎Amesisitiza kuwa Serikali inapaswa kusikiliza kero za wananchi na kuhakikisha changamoto zinazowakabili zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati.‎‎

WANANCHI WASHUKURU AUWSA‎‎

Kwa upande wao, wananchi wa Matevesi wameeleza kuridhishwa na hali ya huduma ya maji katika eneo hilo, wakishukuru AUWSA kwa kuchukua hatua za haraka baada ya kupokea malalamiko yao kuhusu ukosefu wa huduma hiyo.‎‎

Mmoja wa wananchi hao, Loy Lolusu, amesema anashukuru AUWSA kwa kuitikia changamoto hiyo na kuifanyia kazi kwa wakati, hatua ambayo imewezesha huduma ya maji kurejea na kuimarika.‎‎

Amesema changamoto ya ukosefu wa maji katika eneo hilo ilichangiwa kwa kiasi kikubwa na ujenzi wa barabara, uliosababisha usumbufu katika miundombinu ya maji na kuathiri upatikanaji wa huduma kwa wananchi.‎‎

“Tunawashukuru AUWSA kwa kushughulikia changamoto hii kwa wakati tangu tulipowasilisha malalamiko yetu. Tatizo lilianza wakati wa ujenzi wa barabara ambapo miundombinu ya maji iliathirika, lakini kwa sasa hali imetengenezwa na huduma imeimarika,” amesema.‎‎

Amesema kurejea kwa huduma ya maji kumewapunguzia wananchi usumbufu waliokuwa wakipata na kuwawezesha kuendelea na shughuli zao za kila siku kwa utulivu.‎‎

MWENYEKITI MATEVESI AIPONGEZA AUWSA

‎‎Mwenyekiti wa Matevesi, Kassim Kivuyo, amesema kwa sasa huduma ya maji katika eneo hilo inaendelea kutolewa kama kawaida, akieleza kufurahishwa na hatua zilizochukuliwa na AUWSA baada ya wananchi kuwasilisha malalamiko yao.‎‎

Kivuyo amesema tangu changamoto hiyo iliposhughulikiwa, hawajawahi kukumbana tena na tatizo kubwa la huduma ya maji, jambo ambalo amesema limewafariji wananchi pamoja na viongozi wa eneo hilo.‎‎“Sasa yapo na huduma inaendelea kutolewa kama kawaida.

Bahati nzuri, hawa watu wa idara ya maji tangu siku zile hatujawahi kupata changamoto tena. Mimi mwenyewe nimefarijika pamoja na viongozi wenzangu, kwa sababu tumekuwa na mahusiano mazuri na hawa jamaa wa idara ya maji,” amesema Kivuyo.‎‎

Hata hivyo, amesema bado kuna maeneo mengine katika Matevesi ambayo hayajafikiwa kikamilifu na huduma ya maji, akieleza kuwa tayari AUWSA imeanza kuweka mikakati ya kuyafikia maeneo hayo.

‎‎Amesema Mkurugenzi mpya wa AUWSA pamoja na watumishi wake wamempa ahadi ya kuendelea na upanuzi wa mtandao wa maji, ikiwemo mradi wa takribani kilomita 1.5 utakaosaidia kuwafikishia huduma wananchi ambao bado hawajafikiwa.‎‎

Kwa mujibu wa Kivuyo, pia kuna mpango wa kuchimba kisima kitakachosaidia kuunganisha maeneo ya vitongoji vya mwisho ndani ya kijiji hicho, ikiwemo Kitongoji cha Ong’oswa na Orikaria.‎‎

Amesema ombi la kisima hicho liliwasilishwa tangu mwaka jana na AUWSA imeeleza kuwa taratibu za utekelezaji zimefanyika, huku ujenzi wake ukitarajiwa kuanza.

‎‎“Kuna maeneo mengine ambayo yalikuwa bado, lakini kwa bahati nzuri Mkurugenzi mpya pamoja na watumishi wake wametupa ahadi ya kuongeza mtandao wa maji. Pia wametuhakikishia kuhusu kisima kitakachounganisha kitongoji cha mwisho ndani ya kijiji chetu na Kitongoji cha Ong’oswa na Orikaria,” amesema.‎‎

Kivuyo ameipongeza AUWSA kwa kuitikia mahitaji ya wananchi na kuonesha utayari wa kushirikiana na viongozi wa eneo hilo katika kutatua changamoto zilizopo.‎‎

Amesema ushirikiano huo unaonesha kuwa changamoto za huduma ya maji zinaweza kutatuliwa kwa ufanisi pale wananchi, viongozi na mamlaka husika wanaposhirikiana kwa karibu.‎‎

Wananchi hao wameendelea kuiomba AUWSA kuimarisha ufuatiliaji wa miundombinu ya maji katika maeneo yanayofanyiwa ujenzi wa barabara ili changamoto kama hizo zinapojitokeza ziweze kutatuliwa kwa haraka.‎‎

Ziara hiyo imekuwa sehemu ya juhudi za Serikali na wadau wa huduma za maji kuhakikisha changamoto zinazowakabili wananchi zinafuatiliwa na kutatuliwa kwa wakati, sambamba na kuimarisha upatikanaji wa maji safi, salama na ya uhakika.‎

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments