Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Philip Mpango, amepongeza utendaji wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kwa kuimarika na kuwa na hali nzuri kifedha, huku akitoa wito wa kuhakikisha mfuko huo unabakia katika mwenendo huo thabiti.

Dk. Mpango alitoa kauli hiyo leo, Agosti 24, 2025, alipotembelea banda la PSSSF katika Maonesho ya ECOs Forum 2025, yanayofanyika pembezoni mwa Mkutano wa Wenyeviti wa Bodi na Wakuu wa Taasisi za Umma kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha AICC, Arusha.
“Mfuko kwa sasa una afya. Hakikisheni hamteteriki tena,” amesema Dk. Mpango mbele ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa PSSSF, Joyce Mapunjo.
Akitoa taarifa kwa Makamu wa Rais, Kaimu Meneja wa Mipango, Tathmini na Ufuatiliaji wa PSSSF, Hugo Mhina, alieleza kuwa mfuko huo kwa sasa uko katika hali nzuri na unaendelea kutoa huduma bora kwa wanachama kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo.
Kwa mujibu wa Mhina, PSSSF imelipa wastani wa shilingi bilioni 75 kila mwezi kwa wastaafu na wanufaika wapatao 175,000, jambo linalodhihirisha uimara wa mfuko huo katika kutekeleza wajibu wake kwa jamii ya Watanzania.




Mfuko wa PSSSF umeendelea kuwa mhimili muhimu kwa ustawi wa wastaafu na familia zao, huku pia ukichangia kwa kiasi kikubwa katika uchumi wa taifa kwa kulipa mafao kwa wakati na kuhakikisha haki za wanachama wake zinalindwa.Kwa mujibu wa wataalamu wa sekta ya hifadhi ya jamii, kuimarika kwa PSSSF ni hatua muhimu ya kuimarisha imani ya wanachama, kuongeza usajili mpya na kukuza uthabiti wa sekta ya hifadhi ya jamii nchini.
Kauli ya Makamu wa Rais Dk. Mpango ni ishara ya matumaini na uthibitisho kuwa PSSSF iko katika mwelekeo sahihi. Wanachama na wastaafu wanahimizwa kuendelea kuwa na imani na mfuko huo, huku serikali ikiahidi kuusimamia na kuhakikisha unaendelea kuwa na afya njema.




Endelea kutembelea tovuti yetu kwa taarifa zaidi kuhusu PSSSF, mafao ya wastaafu na maendeleo ya sekta ya hifadhi ya jamii Tanzania.




