Friday, November 7, 2025
spot_img
HomeMichezoKabwana FC, Rorya Utd zatangulia robo fainali Umoja Cup Rorya 2025

Kabwana FC, Rorya Utd zatangulia robo fainali Umoja Cup Rorya 2025

Timu ya Kabwana FC na Rorya United zimejikatia tiketi ya kutangulia robo fainali ya michuano ya Umoja Cup Rorya 2025, baada ya mwishoni mwa wiki kuzididimiza Mafundi FC na Kirengo FC.

Kabwana FC imetinga hatua hiyo baada ya Jumamosi iliyopita kuisukumiza nje Mafundi FC kwa mabao 2-1 wakati Jumapili Rorya United wakiifurusha nje ya mashindano Kirengo fc kwa mikwaju ya penalti 8-7 baada ya dakika 90 za mchezo kumalizika kwa suluhu.

Leo utashuhudiwa mchezo mwingine mkali wa hatua ya 16-bora kusaka timu nyingine  itakayoungana na miamba hiyo, pale Samary FC itakaposhuka katika Uwanja wa Maji Sota kumenyana na Shirati Mji.  

Katika mashindano hayo yaliyoanza kutimua vumbi tangu Agosti 10, mwaka huu, jumla ya timu shiriki zilikuwa 20 ambapo tano zilizotolewa kwenye michuano hiyo inayofanyika kila mwaka wilayani hapa, ikiwa na lengo la kudumisha mshikano, amani na kuibua vipaji.

Timu zilizotinga hatua ya 16-bora inayoendelea kwa sasa ni Bubombi FC, Bweru FC, Masonda FC, KMT FC, Kirengo FC, Shirati Mji FC na Mafundi FC ambazo Jumamosi na Jumapili zilitupwa nje ya mashindano na Kabwana FC na Rorya United.

Zingine zilizotinga hatua hiyo ni Kirumba FC, Y Boys FC, Samary FC, Wanamaji FC, Bukura FC, Rifa FC na Gonga FC.

Kwa mujibu wa ratiba ya michuano hiyo baada ya mechi ya leo kati ya Samary FC na Shirati Mji, hatua hiyo ya 16-bora itaendelea tena kesho wakati KMT FC itakapovaana na Young Boys, huku keshokutwa Rifa FC ikiwa na kibarua kigumu dhidi ya Bubombi FC.

Ratiba hiyo itaendelea Jumamosi kwa Bukura FC kuvaana na Bweru FC, kabla ya Msonga FC na Wanamaji FC, kuhitimisha hatua ya 16-bora zitakapomenya Jumapili wiki hii, mechi zote zitapigwa katika Uwanja wa Maji Sota.

Katika mashindano hayo ya Umoja Cup yanayofanyika kila mwaka chini ya Mdhamini Mkuu, Peter Owino, mwaka huu yamekuja kivingene kwa maana ya zawadi mbalimbali kuongezeka kwa timu.

Kwa mujibu wa Katibu wa Mashindano hayo, Telly James, mshindi wa kwanza anatarajiwa kuondoka na kitita cha Sh. 600,000, jezi seti moja yenye thamani ya Sh. 224,000 na mpira wenye thamani ya Sh. 50,000/ pamoja na kombe lenye thamani ya Sh. 300,000.

Mshindi wa pili ataondoka na Sh. 400,000, jezi seti moja yenye thamani ya Sh. 224,000 na mpira wenye thamani ya Sh 50,000 huku mshindi wa tatu naye akipata zawadi kama hizo, lakini kwa upande wa fedha yeye akiondoka na Sh. 150,000.

Kwa upande wa mshindi wa nne yeye ataambulia jezi seti moja yenye thamani ya Sh. 224,000 na mpira mmoja wenye thamani ya Sh. 50,000 tu.

“Sambamba na zawadi hizo, pia mchezaji bora, timu yenye nidhamu, mfungaji  bora, kipa bora, mchezaji bora chipukizi na wengine wengi watakuwa na zawadi zao,” alisema.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments