Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) imesema itaendelea kushirikiana na Sekretarieti za Mikoa na Halmashauri nchini kuimarisha utekelezaji wa Mfumo wa Stakabadhi za Ghala (WRS), kuongeza tija kwa wakulima na kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Mkurugenzi Mtendaji wa WRRB, Asangye Bangu, amesema hayo Agosti 18, 2026, wakati akizungumza na Maafisa Biashara katika Kikao cha Tatu cha Wizara ya Viwanda na Biashara na Maafisa Biashara kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete, Dodoma.
Bangu amesema utekelezaji wenye tija wa mfumo huo unahitaji ushirikiano wa karibu na Maafisa Biashara, hususan katika kusimamia shughuli za maghala na minada ya mazao inayofanyika katika maeneo yao.

Amesema Maafisa Biashara wana nafasi muhimu katika kuhakikisha taarifa sahihi kuhusu mahitaji ya maghala zinapatikana, pamoja na kufuatilia hali, matumizi na uhitaji wa maghala katika mikoa na halmashauri.
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mahusiano kwa Umma na Mawasiliano wa WRRB, Dionis Musseru, amesema elimu kwa umma imeendelea kuongeza uelewa na ushiriki wa wadau katika mfumo huo.
Amesema hadi sasa mazao 11 yanauzwa kupitia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala.






