Friday, November 14, 2025
spot_img
HomeHabariMradi wa Umeme Iringa–Zambia wafikia asilimia 83, kukamilika Mei 2026

Mradi wa Umeme Iringa–Zambia wafikia asilimia 83, kukamilika Mei 2026

Imeelezwa kuwa mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 400 kutoka Iringa hadi Zambia kupitia Tunduma (TAZA) umefikia asilimia 83.45 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Mei 2026, hatua itakayofungua soko jipya la biashara ya umeme barani Afrika.

Akizungumza leo Oktoba 23, 2025, katika eneo la Iganjo mkoani Mbeya wakati wa ziara ya kukagua utekelezaji wa mradi huo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dk. James Mataragio, alisema mradi wa TAZA ni muhimu kwa Taifa kwani utaunganisha Tanzania na nchi za ukanda wa Kusini mwa Afrika (Southern Africa Power Pool) na pia kuimarisha muunganiko wa ukanda wa Mashariki mwa Afrika (East Africa Power Pool).

“Nimshukuru na kumpongeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutenga fedha kwa ajili ya miradi mikubwa ya nishati. Kupitia mradi huu, tutaimarisha biashara ya kuuza na kununua umeme kati ya nchi za Mashariki mwa Afrika na zile za Kusini mwa Afrika,” alisema Dk. Mataragio.

Kuhusu biashara ya kikanda ya umeme, Dk. Mataragio alisema Tanzania tayari imeunganisha gridi yake na nchi za Kenya, Rwanda, Burundi na Ethiopia kupitia mfumo wa East Africa Power Pool, na mipango ipo kuunganisha gridi hiyo na nchi za Kaskazini na Magharibi mwa Afrika.

“Tunaendelea kutekeleza mpango wa kuhakikisha zaidi ya Waafrika milioni 600 wanaopungukiwa na umeme wanapatiwa huduma hii muhimu,” aliongeza.

Akizungumzia mradi wa TAZA, Dk. Mataragio alisema unatekelezwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo wakiwemo Benki ya Dunia, Umoja wa Ulaya na Shirika la Maendeleo la Ufaransa, kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 584.

Amefafanua kuwa mbali na kuunganisha gridi za umeme za nchi za Kusini mwa Afrika, mradi huo utaunganisha pia Mkoa wa Rukwa na umeme wa gridi, sambamba na kuboresha upatikanaji wa nishati hiyo katika mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya na Songwe.

Baada ya kukagua mradi huo, Dk. Mataragio aliliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kumsimamia kwa karibu mkandarasi husika, hususan katika kipindi cha mvua, ili hatua za awali za ujenzi wa misingi (foundation) zikamilike kwa wakati, na kuhakikisha vifaa vyote vinapatikana katika eneo la mradi.

Katika hatua nyingine, Dk. Mataragio aliagiza TANESCO kuhakikisha inapeleka umeme katika eneo la Ngozi ambako unatekelezwa mradi wa kuzalisha umeme kwa jotoardhi, ili mitambo ya uhakiki wa jotoardhi isiendelee kutumia mafuta ya dizeli.

Katika ziara hiyo, Dk. Mataragio aliambatana na Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga, pamoja na watendaji wa Wizara ya Nishati na TANESCO.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments