📌 Ikiwezesha mikopo ya zaidi ya Shilingi bilioni 700 kote nchini
Watu Credit (Tanzania) Limited imeadhimisha miaka mitano tangu kuanza shughuli zake nchini Tanzania, ambapo hadi sasa imehudumia zaidi ya wateja milioni moja na kupanua huduma zake hadi kufikia mikoa 26 kote nchini.
Tangu kuanzishwa kwake jijini Dar es Salaam mwaka 2021, Watu credit Tanzania imewezesha ununuzi wa pikipiki na bajaji zaidi ya 70,000 na simu janja zaidi ya milioni 1.5, ikitoa zaidi ya shilingi bilioni 700 kwa ajili ya kuimarisha usafiri, mawasiliano, ujasiriamali na kuongeza kipato kwa wananchi.
Maadhimisho ya miaka mitano ya Watu credit Tanzania yalifanyika jijini Dar es Salaam chini ya Kaulimbiu “Kila Mtu Ni Watu,” na kuwakutanisha viongozi wa serikali, washirika wa maendeleo, wateja, wadau wa biashara, wanahabari na wafanyakazi wa Watu Tanzania ambapo kwa pamoja walitafakari mchango wa kampuni hii katika kuboresha maisha ya Watanzania.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Meneja wa Watu Credit Tanzania Rumisho Shikonyi, alisema mafanikio haya yanadhihirisha dhamira ya dhati ya kampuni ya kufikisha huduma na fursa za kifedha kwa Watanzania wengi zaidi.
“Miaka mitano iliyopita, Watu Tanzania ilianza ikiwa na imani moja rahisi kwamba, upatikanaji wa fursa haupaswi kutatizwa na ukosefu ama uhaba wa huduma za kifedha. Leo, imani hiyo imekuwa dhahiri, na sasa imegeuka kuwa biashara ya kitaifa inayohudumia wateja kote Tanzania na kuwawezesha watu wengi zaidi kupata nyenzo wanazohitaji kwa ajili ya uzalishaji, kuwasiliana na kujenga maisha bora,” alisema.

Mwenyekiti wa Bodi ya Watu credit Tanzania Bhavin Parmar, alisema miaka mitano ya kwanza ya kampuni hii imeweka msingi imara wa ukuaji endelevu unaozingatia uwajibikaji.
“Kama Bodi, tunajivunia mafanikio ambayo Watu credit Tanzania imeyapata katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. Ukuaji huu unaambatana na wajibu, na ni jukumu letu sasa kuhakikisha kuwa ubunifu unaendana na uwajibikaji, malengo makubwa yanaongozwa na uadilifu, na kila uamuzi unaongeza thamani ya kudumia wateja wetu, washirika, wafanyakazi na jamii tunazozihudumia. Tunaingia katika hatua inayofuata kwa kujiamini kutokana na uongozi wetu, washirika wetu, watu wetu na mustakabali wa Tanzania,” alisema.
Mfumo wa utoaji huduma wa Watu Tanzania unaunganisha matumizi ya teknolojia na mtandao mpana wa mawakala wa ndani ili kufanya huduma za mikopo kuwa rahisi kufikiwa, kueleweka na kusimamiwa. Wateja wanaweza kufanya marejesho ya mikopo bila kutumia fedha taslimu kupitia huduma za fedha kwa njia ya simu pamoja na Programu ya Watu (Watu App), kulingana na ratiba za kila siku, wiki na mwezi.

Kutoka kushoto ni Msimamizi wa Mdahalo, Khalila Mbowe; Meneja wa Nchi, Watu Tanzania, Rumisho Shikonyi (wa pili kushoto) Meneja Mkuu wa Uendeshaji, Watu Tanzania, Abdallah Mohamed (katikati), Mkuu wa Mahusiano ya Serikali wa Watu Group, Erick Massawe wa pili Kulia na Mkuu wa Kitengo cha Huduma za simu, Samsung Tanzania, Mgope Kiwanga (kulia). Hafla hii ilifanyika tarehe 29 Juni 2026, jijini Dar es salaam.
Mbali na kutoa huduma za kifedha kwa wateja, Watu Tanzania pia imechangia katika kuongeza fursa za ajira na uongozi. Kwa sasa kampuni ina wafanyakazi zaidi ya 500 nchini kote, huku wanawake wakichangia takribani asilimia 43 ya nguvu kazi na kushika karibu nusu ya nafasi zote za uongozi.
Katika hafla hiyo, Watu credit Tanzania ilitoa shukrani za dhati kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mamlaka za udhibiti, mamlaka za serikali za mitaa, taasisi za kifedha, wazalishaji, waendeshaji wa mitandao ya simu, wafanyabiashara, washirika wa teknolojia, wateja pamoja na wafanyakazi wake kwa mchango wao katika safari ya mafanikio ya kampuni kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Wakati Watu credit Tanzania inapoanza hatua mpya ya ukuaji, kampuni inaendelea kujizatiti kupanua upatikanaji wa rasilimali za uzalishaji, kuwekeza katika teknolojia, kuimarisha ushirikiano, na kuleta suluhisho inayowasaidia Watanzania.





