HomeHabariSpika Zungu aimwagia serikali ‘maua yake’ kutokana na Bajeti ya viwango

Spika Zungu aimwagia serikali ‘maua yake’ kutokana na Bajeti ya viwango


Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mussa Azzan Zungu, ameipongeza Serikali inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kukubali kufanya marekebisho ya baadhi ya tozo na kodi zilizopendekezwa katika Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2026, hatua aliyosema imezingatia maslahi mapana ya wananchi na wafanyabiashara.

Amesema hayo leo Juni 25, 2026 Bungeni jijini Dodoma alipohitimisha mjadala wa Muswada huo ambao umepitishwa kwa kishindo na wabunge, ukitarajiwa kuiwezesha Serikali kukusanya na kutumia takribani shilingi trilioni 62.33 katika mwaka wa fedha 2026/2027.

Spika Zungu amesema mchakato wa kupitisha Muswada huo umefanyika kwa utulivu kutokana na majadiliano ya kina kati ya Serikali na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, hatua iliyosaidia kufikia mwafaka katika maeneo mbalimbali ya kodi na tozo.

Amesema miongoni mwa marekebisho yaliyokubaliwa na Serikali ni pamoja na kuondolewa kwa pendekezo la kuwatoza kodi wafanyabiashara wapya kabla hawajaanza biashara, ambapo sasa wataruhusiwa kufanya biashara kwa mwaka mmoja bila kodi.

Aidha, amesema Serikali imefuta pia pendekezo la kutoza ushuru wa bidhaa kwa asilimia 5 kwa pikipiki, hatua inayolenga kuwapunguzia mzigo wananchi hususan vijana wanaotumia vyombo hivyo katika shughuli zao za kiuchumi.

Vilevile, Spika Zungu amesema Serikali imepunguza kiwango cha ushuru wa bidhaa kwa magari yaliyotumika kutoka asilimia 20 iliyopendekezwa hadi asilimia 18, badala ya asilimia 15 ya awali, hatua inayozingatia mazingira ya soko.

Ameongeza kuwa Serikali pia imeondoa pendekezo la kutoza kodi ya zuio kwa asilimia 1 kwenye mazao ya kilimo, mifugo, maziwa, samaki na mazao mengine ya kijamii na kiuchumi, ili kuimarisha sekta hizo zinazotegemewa na wananchi wengi.

Katika hatua nyingine, Spika Zungu ameitaka Serikali kuendelea kudhibiti matumizi yasiyo ya lazima, ikiwemo ununuzi wa magari ya kifahari, ili kuelekeza rasilimali zaidi kwenye miradi ya maendeleo ya wananchi.

Kwa upande wake, Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, amesema bajeti ya mwaka 2026/2027 itagharamiwa kwa kiasi kikubwa na mapato ya ndani, ambayo yanatarajiwa kufikia asilimia 74.2 ya bajeti yote.

Amesema Serikali pia itakopa jumla ya shilingi trilioni 15.54, ambapo mikopo ya ndani na nje yenye masharti nafuu pamoja na ya kibiashara itatumika kufadhili nakisi ya bajeti inayokadiriwa kufikia shilingi trilioni 7.71.

Baada ya kupitishwa kwa Muswada huo na Bunge, sasa hatua inayofuata ni Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuuridhia na kuutia saini ili Sheria ya Fedha ya mwaka 2026 ianze kutumika rasmi kuanzia Julai Mosi, 2026.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments