DODOMA: Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Jaji wa Mahakama ya Rufani Jacobs Mwambegele, amewataka watendaji wa uchaguzi kuheshimu viapo vyao na kutekeleza majukumu kwa kuzingatia Katiba, sheria na kanuni ili kuhakikisha mchakato wa uchaguzi unaendeshwa kwa uadilifu.
Mwambegele ametoa wito huo Novemba 2, 2026, katika Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, mkoani Dodoma, wakati wa kufunga mafunzo ya watendaji watakaosimamia uchaguzi mdogo wa ubunge katika Jimbo la Chamwino na uchaguzi wa madiwani katika kata 11 za Tanzania Bara.
Amesema watendaji hao wanapaswa kuzingatia Katiba, sheria za uchaguzi, kanuni za maadili ya uchaguzi na maelekezo yanayotolewa na Tume katika kipindi chote cha uchaguzi.




“Ninawasisitiza kuheshimu viapo vyenu kwa nafasi mlizoteuliwa, tekelezeni majukumu yenu kwa kuzingatia Katiba ya Nchi, sheria za uchaguzi na kanuni zake, kanuni za maadili ya uchaguzi na maelekezo mbalimbali yanayotolewa na yatakayotolewa na Tume katika kipindi hiki cha uchaguzi,” amesema.
Aidha, amewataka watendaji hao kutotegemea uzoefu pekee katika kusimamia uchaguzi, bali kuzingatia taratibu za kila uchaguzi kwa kuwa mazingira na mahitaji yake hutofautiana.
Amesema hata wale wenye uzoefu wa kusimamia chaguzi zilizopita wanapaswa kuepuka kufanya kazi kwa mazoea na kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa kufuata maelekezo ya Tume.
Uchaguzi huo mdogo unatarajiwa kufanyika Novemba 4, 2026, ukihusisha Jimbo la Chamwino na kata 11 za Tanzania Bara.
Kata hizo ni Nonde katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya; Lugenge, Halmashauri ya Mji wa Njombe; Bargish, Halmashauri ya Mji wa Mbulu; Makole, Halmashauri ya Wilaya ya Muheza; Mwera, Halmashauri ya Wilaya ya Pangani; na Oldonyosambu, Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro.
Nyingine ni Igalula katika Halmashauri ya Wilaya ya Uyui; Shelui, Halmashauri ya Wilaya ya Iramba; Mvumi, Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa; Nyarero, Halmashauri ya Wilaya ya Tarime; na Ilolangulu, Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe.





