Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anamringi Macha amewataka viongozi wa dini kuwa chachu ya umoja na mshikamano miongoni mwa wananchi, akisisitiza umuhimu wa kujitokeza kwa wingi kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu ujao kama haki ya kikatiba.
Amesema hayo leo wakati wa mkutano na viongozi wa dini uliofanyika mkoani humo, uliolenga kuhamasisha wananchi kushiriki kwa amani katika zoezi la upigaji kura.
Kwa upande wake, aliyewahi kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Kanyasu, ametoa wito kwa wananchi na viongozi wa dini kutumia mitandao ya kijamii kwa njia chanya, ikiwemo kuhimiza amani na kuwahamasisha wananchi kujitokeza kupiga kura.
Nao viongozi wa dini waliohudhuria mkutano huo wamependekeza elimu zaidi itolewe kwa wananchi kuhusu jukumu la vyombo vya usalama, wakisisitiza kuwa vikosi hivyo vipo kwa ajili ya kulinda amani na usalama wa wananchi wakati wa mchakato mzima wa uchaguzi.




