Tuesday, May 12, 2026
spot_img
HomeGeneral NewsWaziri Masauni asisitiza matumizi ya nishati safi kupikia

Waziri Masauni asisitiza matumizi ya nishati safi kupikia

Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye kilele cha siku ya mazingira duniani yatakayofanyika Juni 5 katika ukumbi wa Jakaya Kikwete mkoani Dodoma.

Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Hamad Yusuph Masauni alipoongea na waandishi wa habari wakati akitoa tamko la siku ya mazingira duniani.

Alitaja baadhi ya mambo yatakayofanyika kuwa ni  pamoja na uzinduzi wa program ya mageuzi ya kimkakati inayohusu mazingira endelevu 2025-2030 ambayo ni nyenzo utekelezaji wa Dira 2050.

Alisema pia kutakuwa na kongamano kubwa linalotarajiwa kuwashirikisha watu zaidi ya 1,000 kutoka ndani na nje ya nchi na kampuni zaidi ya 100 zitashiriki kwenye maonesho wakati wa kongamano hilo.

Alisema katika shamra shamra za kuelekea kilele cha siku ya mazingira serikali   inatarajia kuzindua mpango mkakati maalum wa mazingira utakaotekelezwa kuanzia mwaka 2026 hadi 2030 katika  kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi na kuimarisha usimamizi wa mazingira nchini.

Masauni, amesema mkakati utaozinduliwa unalenga kushughulikia kwa kina changamoto mbalimbali za kimazingira, ikiwemo taka ngumu mijini, matumizi yasiyo endelevu ya ardhi, uharibifu wa mazingira na usimamizi wa mifumo ya uzalishaji. 

Amesema mpango huo utaelekezwa katika maeneo yote muhimu bila kuacha sekta yoyote nyuma, ukiwemo upandaji miti, usimamizi wa mifugo, udhibiti wa taka za plastiki pamoja na uimarishaji wa mifumo ya mazingira mijini na vijijini.

Waziri Masauni amebainisha kuwa Serikali pia imejipanga kuimarisha taasisi zinazosimamia mazingira ili ziwe na uwezo wa kutosha kiutendaji, wataalamu wenye weledi na rasilimali za kutosha katika kuhakikisha utekelezaji wa majukumu yao unafanyika kwa ufanisi na kuwa endelevu. 

Amesema mageuzi yatayofanyika ni sehemu ya jitihada za kuhakikisha nchi inakuwa na mfumo imara wa usimamizi wa mazingira unaoweza kukabiliana na changamoto zilizopo na zijazo. 

Aidha, amesisitiza kuwa Serikali inalenga kubadili taka kuwa fursa ya kiuchumi, ambapo taka zitachakatwa na kutumika kuzalisha bidhaa mbalimbali, ikiwemo nishati na bidhaa za viwandani, hatua itakayosaidia kupunguza uchafuzi wa mazingira na kuongeza tija ya kiuchumi. 

Amesema katika kuelekea maadhimisho hayo kutafanyika makongamano mbalimbali ikiwemo na elimu kwa wananchi ili kuweza kuwa na uelewa wa suala la mazingira. 

Hata hivyo amesema moja ya kongomano litakalofanyika ni katika maadhimisho ya miaka 40 ya Baraza la Usimamizi na Uhifadhi Mazingira (NEMC). 

Amesema katika jitihada zingine Serikali kuendelea kuhamasisha wananchi kupanda miti ambapo kuelekea maadhimisho hayo watapanda Miti Wilayani Kilosa mkoani Morogoro. 

Waziri Masauni alisema uzinduzi rasmi wa mpango huo unatarajiwa kufanyika katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mazingira yatakayofanyika tarehe 5 Juni ambapo Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments