📌Ni kwenye kutoa elimu ya masuala ya Nishati Safi ya Kupikia
📌Wananchi wamejitokeza kwa wingi kujipatia majiko ya bei ya ruzuku ya shilingi 17,500/=
Tanga – Ushiriki wa Wizara ya Nishati pamoja na taasisi zake REA na TANESCO katika Maonesho ya Wiki ya Chakula yamevutia wananchi wengi kutembelea banda la Wizara ili kupata elimu ya nishati safi ya kupikia na taarifa kuhusu miradi ya umeme, gesi asilia na mafuta.
Miongoni mwa waliotembelea maonesho hayo ni Mkurugenzi wa Nishati Safi ya Kupikia kutoka Wizara ya Nishati, Bw. Nolasco Mlay, ambaye alieleza kufurahishwa na muito wa wananchi katika banda la Wizara na taasisi zake.




“Nimevutiwa na muitikio mkubwa wa wananchi wanaofika kuchukua majiko ya gesi kwa bei ya ruzuku ya Sh17,500 yanayotolewa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) pamoja na kupewa elimu. Hakika mwamko huu unatia moyo katika kutekeleza Ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia hapa Tanga,” alisema Mlay.


Mlay pia aliwatahadharisha wananchi kutumia nishati safi kwa sababu ni salama kiafya na kwa mazingira, huku akisisitiza kwamba Serikali inaendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi kwa makundi mbalimbali, ikiwemo taasisi zinazolisha watu zaidi ya 100.
Lengo la Serikali ni kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034, hatua itakayochangia afya bora, usalama wa mazingira na kupunguza utegemezi wa nishati chafu.




