Msanii wa muziki Zuchu, kwa kushirikiana na CRDB Bank Foundation, amezindua rasmi darasa la kwanza la Zuchu Imbeju Masterclass, likiwakutanisha zaidi ya vijana 300 wanaojihusisha na sekta ya muziki, wakiwemo waimbaji, madansa, waandaaji wa muziki na mameneja wa wasanii.
Darasa hilo la siku tano linalenga kuwajengea washiriki maarifa na ujuzi wa kitaaluma utakaowasaidia kukuza vipaji vyao na kujiendesha kwa mafanikio katika tasnia ya burudani. Aidha, mshiriki atakayefanya vizuri zaidi atapata fursa ya kufanya kazi moja kwa moja na Zuchu.
Akizindua mafunzo hayo, Mkuu wa Uendeshaji wa CRDB Bank Foundation, Joycelean Makule, alisema programu hiyo inalenga kuunganisha vipaji vya wasanii na fursa za maendeleo ya kisekta, sambamba na kuwapatia elimu ya fedha, uwekezaji na matumizi ya uchumi wa kidijitali ili kuwawezesha kujenga msingi imara wa kiuchumi.



Kwa upande wake, Zuchu alisema mtaala wa darasa hilo unajumuisha mada muhimu zinazomhusu msanii wa kisasa, ikiwemo sheria za mikataba, namna ya kutambua mikataba yenye manufaa, matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii katika kutangaza na kusambaza kazi za sanaa, pamoja na elimu ya fedha na uwekezaji inayotolewa na CRDB Bank Foundation.
Zuchu aliishukuru CRDB Bank Foundation na wadau wengine kwa kufanikisha mpango huo, huku akitoa shukrani maalumu kwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuunga mkono mradi huo kupitia ufadhili wa vijana 180 kushiriki katika mafunzo ya Zuchu Imbeju Masterclass.






