Diwani wa Kata ya Masama Kusini, Mhe. Cedrick Benjamini Pangani, ameonesha kukerwa na ubovu wa jiko la kupikia chakula cha wanafunzi katika Shule ya Msingi Nkwamakuu na kuahidi kulibomoa na kujenga jiko jipya kwa ajili ya kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.
Ahadi hiyo imetolewa wakati wa ziara yake katika Kitongoji cha Nkwamakuu kilichopo Kata ya Masama Kusini, Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, ambapo wananchi walipata fursa ya kuwasilisha changamoto mbalimbali zinazowakabili kwa kipindi kirefu.
Wananchi wa kitongoji hicho wameishukuru Serikali kwa kuwasikiliza na kuahidi kutoa ushirikiano wa karibu katika kutatua changamoto zao. Miongoni mwa changamoto zilizowasilishwa mbele ya Diwani ni uchakavu wa miundombinu katika Shule ya Msingi Nkwamakuu, ikiwemo ubovu wa jiko la kupikia chakula cha wanafunzi, vyoo, stoo, pamoja na uhitaji wa darasa moja kwa ajili ya wanafunzi wa Darasa la Pili ambao kwa sasa wanapokezana darasa na wanafunzi wa Darasa la Kwanza.




Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Nkwamakuu, Ndugu Jorome Lema, ameiomba Serikali kuitazama shule hiyo kwa jicho la ukarabati wa majengo na uboreshaji wa huduma za msingi ili kuendelea kuongeza kiwango cha ufaulu. Aidha, amewataka wananchi pamoja na wakazi wa maeneo jirani kuwa walinzi wa mali za shule na kuzuia mifugo kuingia katika eneo la shule.
Akizungumza baada ya kupokea changamoto hizo, Diwani Pangani amekiri kuwepo kwa ubovu mkubwa wa jiko la shule, akisema limekuwa kero kwa muda mrefu. Ameeleza kuwa jiko hilo litabomolewa na kujengwa upya kwa kushirikiana na wadau mbalimbali pamoja na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Hai.

Aidha, amesisitiza kuwa utunzaji wa mazingira ni jukumu la kila mwananchi, akiwataka wananchi kuhakikisha wanatunza miti inayopandwa katika maeneo ya shule na kuacha kulisha mifugo ndani ya maeneo hayo.
Katika hatua nyingine, Pangani amewapongeza walimu na wafanyakazi wa Shule ya Msingi Nkwamakuu kwa juhudi kubwa wanazozifanya katika kutoa elimu, akisema taaluma ya ualimu ni wito kutoka kwa Mungu. Pia amezungumza na wanafunzi wa shule hiyo, akiwahimiza kujisomea kwa bidii ili kuendelea kukuza ufaulu wa shule hiyo.









