Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeanza kuchukua hatua ya utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa wakati wa kampeni wilayani Karatu mkoa wa Arusha ya kuitaka TRA kuongeza wigo wa utoaji huduma.
Kamishna Mkuu wa TRA Yusuph Mwenda akiwa ziarani Karatu jana Februari 14,2026 amesema, wakati wa kampeni za uchaguzi 2025 Rais Dk. Samia aliahidi kuongeza wigo wa huduma za kodi ndani ya siku 100 na kuwa hatua za utekelezaji ndiyo zimeanza.
Kamishna Mwenda amesema kuwa, katika hatua za awali za utekelezaji wa maagizo ya Rais Dk. Samia amekutana na kufanya mazungumzo na Wafanyabiashara mbalimbali wakiwemo waendeshaji wa shughuli za utalii kabla ya kufanya maamuzi ya aidha kuanzisha mkoa wa kodi au kupanua huduma ambapo pia amefanya mazungumzo na Mkuu wa wilaya ya Karatu Dk. Lameck Karanga.


Kamishna Mkuu Mwenda amesema TRA itaendelea kuwapatia huduma bora walipakodi kote nchini wakiwemo wa Wilaya Karatu na kuwa itaendelea kuwasikiliza na kutatua changamoto zao.
”Napenda kuwahakikishia walipakodi wote kwamba tutaendelea kuwezesha biashara zenu na kuwapa huduma bora huku tukitumia zaidi mifumo ya kidijitali ikiwemo IDRAS” amesema Mwenda.
Aidha Kamishna Mkuu Mwenda amesema TRA itaendelea kutoa elimu ya kodi mara kwa mara kwa walipakodi Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Karatu Dk. Lameck Karanga amesema wamefurahishwa na ujio wa Kamishna Mkuu kwenye eneo lao na kuwa wilaya anayoiongoza ina uchumi mkubwa ambao unaotokana na shughuli za utalii.


Amesema wamekuwa wakishirikiana na TRA katika masuala mbalimbali ya kodi hali iliyowezesha kuvuka malengo ya makusanyo kwa miezi yote. Kwa upande wa wafanyabiashara waliokutana na Kamishna Mkuu, Mwenyekiti wa umoja wa waendesha shughuli za utalii mkoani Arusha (TATO) Wilbard Chambulo amepongeza utendaji kazi wa TRA ambao umeisogeza karibu na wananchi hali ambayo imeongeza makusanyo ya Kodi kwa wilaya ya Karatu.
Amesema wafanyabiashara wa mji wa Karatu wapo tayari kulipa kodi kwa hiari na kupongeza mfumo mpya wa usimamizi wa mapato ya ndani wa IDRAS ambao ni wiki moja sasa tangu uanze kufanya kazi lakini tayari wameanza kuonja matunda yake kupitia huduma zinazotolewa na mfumo huo.
Amesema mfumo wa IDRAS utakuwa muarobaini wa changamoto nyingi za kikodi ikiwemo kuokoa myda wa walipakodi kwenda kufuata huduma za kodi TRA.
”Kupitia mfumo huu kutakuwa na usawa katika ukadiriaji wa kodi maana mfumo huu ni wa uwazi na unaonyesha mauzo, manunuzi na faida hivyo Mlipakodi atapata faida yake na TRA watapata kodi yao” amesema Chambulo.
Kuhusu ukwepaji kodi Chambulo amesema wanaokwepa kodi kwa kutokutoa risiti hawana nafasi kwenye sekta ya utalii ambapo wamekuwa wakiwatenga katika kuwapa huduma za manunuzi ya vitu mbalimbali hali inayowalazimu nao kuanza kutoa risiti.
Naye Esther Dominic akizungumza katika kikao hicho amesema IDRAS itasaidia kuokoa muda wao na kuwa shughuli nyingi zimerahisishwa ikiwe kuomba TIN mtandaoni na kupata Tax Clearance.
Akiwa Karatu Kamishna Mkuu Mwenda aliwatembelea baadhi ya Walipakodi akiwemo Gibbs Farm ambapo msimamizi wa fedha George Seostine amemshukuru Kamishna Mkuu kwa kuwatembelea na kuwasikiliza na kuipongeza TRA kwa kuanzisha mfumo wa IDRAS ambao utakuwa tiba ya changamoto za Kodi.Seostine ameahidi kuendelea kutoa ushirikiano zaidi kwa TRA ili kuwawezesha kukusanya zaidi na kuisaidia nchi kupata fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo.





