Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dorothy Gwajima, amewataka wanawake wanaofanya kazi katika Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuwa vinara wa mabadiliko katika kufanikisha ajenda ya taifa ya matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Akizungumza katika Kongamano la Pili la Wanawake la Nishati Safi ya Kupikia kwa Umeme lililoandaliwa na wanawake wa TANESCO, Waziri Gwajima amesema wanawake hao wana nafasi ya kipekee ya kuhamasisha jamii kuachana na matumizi ya kuni na mkaa na badala yake kutumia umeme kama nishati safi, salama na nafuu.
Ameeleza kuwa takwimu zinaonesha asilimia 81 ya kaya nchini bado zinatumia nishati isiyo safi ya kupikia, hali inayowaathiri zaidi wanawake kiafya, kiuchumi na kijamii. Amebainisha kuwa wanawake ndio wahanga wakuu wa madhara ya moshi wa kuni na mkaa, ikiwemo magonjwa ya mfumo wa hewa pamoja na kupoteza muda mwingi kutafuta nishati hiyo.
Kutokana na hali hiyo, amewataka wanawake wa TANESCO kuanzia mabadiliko hayo majumbani mwao kwa kutumia majiko ya umeme ili wawe mfano halisi kwa jamii.




Dk. Gwajima amesisitiza kuwa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034. Amesema lengo hilo haliwezi kufikiwa bila ushiriki wa sekta zote, akiitaja TANESCO kuwa mhimili muhimu katika kuhakikisha umeme unatumika kikamilifu kuboresha maisha ya wananchi, hususan wanawake.
Aidha, amewahimiza wanawake wa shirika hilo kuwa mabalozi wa mabadiliko katika familia na jamii kwa kuondoa dhana potofu kuwa umeme ni ghali kwa matumizi ya kupikia. Amefafanua kuwa maendeleo ya teknolojia yameleta majiko yanayotumia umeme kidogo na yenye gharama nafuu, hivyo hakuna sababu ya kuendelea kung’ang’ania nishati zinazoharibu afya na mazingira.
Pia ametoa wito kwa wanawake wa TANESCO kushirikiana na maafisa maendeleo ya jamii na wadau wengine kueneza elimu kuhusu faida za nishati safi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Lazaro Twange, amesema nafasi ya wanawake ndani ya shirika hilo inaheshimika na kuthaminiwa katika ngazi zote za uongozi, hivyo aliwataka kuendelea kuwa makini na kudumisha mshikamano.

Ameongeza kuwa uongozi wa TANESCO unatambua mchango wa wanawake katika safari ya kulifikisha shirika mbele zaidi, akibainisha kuwa hakuna wakati suala la kupandishwa vyeo au utoaji wa fursa limekuwa likipuuzwa bila kuzingatia usawa wa kijinsia. Aliwahakikishia wafanyakazi wanawake kuwa sauti zao zinasikika na kwamba uongozi utaendelea kusimamia haki na maslahi yao kwa kuzingatia misingi ya usawa na haki kazini.
Katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, Twange amesema TANESCO linaungana na wanawake wengine duniani kuhimiza haki na usawa kwa wanawake na wasichana sambamba na utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya mwaka 2050. Aidha, amegusia ajenda ya nishati safi ya kupikia, akieleza kuwa shirika linaunga mkono juhudi za Serikali zinazoongozwa na Rais Samia katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi.
Amebainisha kuwa TANESCO ina mpango wa kusambaza majiko ya umeme kwa watumishi wake na kuendelea kuhamasisha wananchi kuachana na nishati zisizo salama. Hata hivyo, amesisitiza kuwa shirika litaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali, ikiwemo wizara husika, kuhakikisha ajenda hiyo inatekelezwa kwa vitendo.





