Thursday, March 5, 2026
spot_img
HomeHabariWaziri Nanauka amshukuru Rais Samia kwa kujali maendeleo ya vijana

Waziri Nanauka amshukuru Rais Samia kwa kujali maendeleo ya vijana

Waziri  wa Nchi Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka amewakabidhi pikipiki, bajaji na maguta yenye thamani ya Sh. milioni 140 vijana wa Mkoa wa Mtwara ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Rais Samia Suluhu Hassan kuwainua vijana.

Akizungumza mara baada ya kugawa vifaa hivyo katika hafla ya Jukwaa la Vijana mkoani  Mtwara, Waziri Nanauka alisema kwa kupata vifaa hivyo vijana wamepewa nguvu mpya.

Makabidhiano hayo yalihusisha pikipiki 15, bajaji 5 na maguta 5 vyenye thamani ya jumla ya Sh. milioni 140, ambavyo vitatumika kusaidia shughuli za usafirishaji na kurahisisha utekelezaji wa majukumu ya vijana katika jamii. 

“Kama ambavyo tumefanya kwenye maeneo mengine, mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan aliahidi atawezesha vijana na sisi Wizara kauli mbiu yetu ni kusema na kutenda, tumekabidhi hapa Mtwara vifaa hivi vyenye bima zote,” alisema 

“Tumewapa muda wa miezi mitatu kabla ya kufanya marejesho wajipange, tunafanya kazi kwa ushirikiano na CRDB Foundation tunawakabidhi vifaa tunawafuatilia kuhakikisha wanakua na kuondokana na mikopo ya kausha damu,” alisema 

“Nitoe wito kwa vijana nchini fursa zimeshatolewa ni wajibu wao kuzitafuta na kuzitumia, kazi yetu ni kusema na kutenda sasa yule ambaye amejiandaa ndiye atapata fursa mheshimiwa Rais anataka vijana wamiliki uchumi,” alisema 

Waziri Nanauka alisema hivi sasa serikali inatoa hadi mikopo ya kijana mmoja mmoja tena bila dhamana hivyo aliwataka vijana kuchangamkia fursa hiyo. 

Alisema hatua hiyo inaonyesha wazi kuwa Serikali haizungumzi tu kuhusu kuwawezesha vijana, bali inaweka vitendo mezani kwa kuwapatia rasilimali halisi zinazoweza kubadilisha maisha yao na kuchochea maendeleo ya kiuchumi. 

Alisema  makabidhiano ya vitendea kazi hivyo yamelenga kuimarisha utendaji kazi wa vijana katika sekta ya usafirishaji na huduma za kijamii.

Alisema lengo ni kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku, kurahisisha huduma kwa wananchi, hasa katika maeneo yenye changamoto za usafiri. 

Alitaja lengo lingine kuwa ni kupanua fursa za ajira na kipato kwa vijana wa Mkoa wa Mtwara kwa kuwapatia zana hizo, vijana wanapewa nafasi ya kujitegemea kiuchumi na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo. 

“Mpango huu una manufaa makubwa kwa vijana, ikiwa ni pamoja na ajira na kipato Pikipiki, bajaji na maguta ni nyenzo muhimu katika sekta ya usafirishaji ambayo inaajiri vijana wengi hivyo kupitia vifaa hivyo, vijana wanaweza kujipatia kipato cha kila siku na kuboresha maisha yao,” alisema.

Aidha, alisema kwa kupewa dhamana ya kusimamia na kutumia vitendea kazi hivyo, vijana wanajifunza nidhamu ya kazi, usimamizi wa rasilimali na kuwajibika kwa jamii.

“Vijana wanaweza kutumia vifaa hivyo kama msingi wa kuanzisha au kupanua biashara zao za usafirishaji na huduma mbalimbali na manufaa kwa taifa kupitia mpango huo uchumi wa ndani unaimarika kupitia shughuli za usafirishaji na biashara ndogondogo,” alisema. 

Alisema ajira zinaongezeka, hivyo kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana na huduma kwa jamii zinaboreshwa, hasa katika maeneo ambayo usafiri ni changamoto.

Waziri Nanauka alisema mpango huo unasaidia kujenga kizazi cha vijana wenye uwezo, ari ya kazi na mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi. 

Alisema makabidhiano hayo ni ishara kwamba Serikali inaendelea kuwaamini na kuwawekea mazingira mazuri vijana kufanikiwa. 

Hata hivyo, Waziri Nanauka alisema mafanikio ya mpango huo yatategemea pia nidhamu, ubunifu na uwajibikaji wa vijana wenyewe.

“Ni wajibu wa vijana kuhakikisha wanatumia rasilimali hizi walizopata kwa ufanisi ili kuleta mabadiliko chanya katika maisha yao na jamii kwa ujumla,” alisema.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments