Wednesday, March 11, 2026
spot_img
HomeHabariWazabuni Ruvuma, Iringa na Njombe wajengewa uwezo matumizi ya Moduli ya Rufaa

Wazabuni Ruvuma, Iringa na Njombe wajengewa uwezo matumizi ya Moduli ya Rufaa

Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) imewakutanisha wazabuni na taasisi nunuzi kutoka mikoa ya Ruvuma, Iringa na Njombe katika mafunzo maalum ya kuwajengea uwezo kuhusu matumizi ya moduli ya kupokea na kushughulikia malalamiko na rufaa katika mfumo wa kielektroniki wa ununuzi wa umma wa NeST.

Mafunzo hayo yaliyofanyika katika miji ya Songea na Iringa yamewahusisha jumla ya washiriki 380 wakiwemo wazabuni, wataalamu wa ununuzi, sheria, TEHAMA pamoja na makundi maalum kama wanawake, vijana, wazee, watu wenye mahitaji maalum na mafundi wa ndani.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Katibu Mtendaji wa PPAA, James Sando amesema mafunzo hayo yanatolewa kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) kwa lengo la kuongeza ufanisi kwa wazabuni na taasisi nunuzi katika utekelezaji wa majukumu yao, hasa katika kushughulikia malalamiko na migogoro inayotokana na michakato ya ununuzi wa umma.

“Mafunzo haya yanalenga kuimarisha utendaji kazi wenu, kuongeza uelewa wa matumizi ya moduli ya kupokea na kushughulikia malalamiko na rufaa katika Mfumo wa Ununuzi wa Umma kwa Njia ya Kielektroniki (NeST),” amesema Sando.

Ameongeza kuwa mafunzo hayo pia yanatekeleza azma ya Serikali ya kuwashirikisha vijana, wanawake na makundi maalum katika shughuli za ununuzi wa umma ili kuwapa uelewa wa michakato hiyo na kusaidia Serikali kupata thamani halisi ya fedha katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati yenye tija kwa taifa.

Sando amewasihi washiriki kutumia fursa hiyo kujifunza kwa kina namna moduli ya kuwasilisha malalamiko na rufaa inavyofanya kazi katika mfumo wa NeST, akieleza kuwa mfumo huo unatoa njia rahisi, ya haraka na yenye uwazi kwa wadau kushiriki katika mchakato wa kushughulikia malalamiko yanayotokana na zabuni za umma.

Amebainisha kuwa matumizi ya moduli hiyo yameongeza ufanisi katika usimamizi wa rufaa, kupunguza muda wa kushughulikia mashauri na kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika utoaji wa haki, hali inayosaidia kuokoa muda na kupunguza gharama zinazohusiana na usuluhishi wa migogoro ya ununuzi.

Kwa upande wake, Meneja wa Usimamizi wa Rufaa na Sheria wa PPAA, Florida Mapunda amesema mafunzo hayo yamelenga kutoa elimu kwa wadau wa ununuzi wa umma kuhusu taratibu sahihi za uwasilishaji na ushughulikiaji wa malalamiko na rufaa kupitia mfumo wa NeST.

Amesema PPAA kwa kushirikiana na PPRA wamejenga moduli maalum katika mfumo huo ili kuwasaidia wazabuni na taasisi za umma kuwasilisha malalamiko na rufaa kwa ufanisi zaidi kupitia mtandao.

Mapunda ameongeza kuwa tangu kuanza kwa matumizi ya moduli hiyo, jumla ya mashauri 596 yamewasilishwa kupitia mfumo wa NeST, jambo linaloifanya PPAA kuendelea kutoa elimu kwa wadau wa ununuzi wa umma ili waweze kuelewa vizuri matumizi ya mfumo huo.

Kupitia mafunzo hayo, washiriki walipewa mada mbalimbali zikiwemo uwasilishaji na ushughulikiaji wa malalamiko na rufaa katika ununuzi wa umma, matumizi ya mfumo wa NeST, utoaji wa tuzo za zabuni, pamoja na taratibu za uandaaji, upekuzi na utiaji saini wa mikataba.

Mada nyingine zilihusu maombi ya kuongezewa muda wa kuwasilisha rufaa nje ya muda pamoja na utaratibu wa kuwasilisha na kushughulikia rufaa katika mfumo wa NeST.

Mafunzo hayo yaligawanyika katika awamu mbili ambapo awamu ya kwanza ilifanyika Songea mkoani Ruvuma tarehe 2 na 3 Machi 2026, huku awamu ya pili ikifanyika Iringa kwa washiriki kutoka mikoa ya Iringa na Njombe tarehe 5 na 6 Machi 2026.

Programu hiyo ni mwendelezo wa mafunzo yaliyowahi kufanyika katika kanda nyingine za nchi zikiwemo Kanda ya Pwani na Kanda ya Ziwa kwa lengo la kuendelea kuwajengea uwezo wadau wa ununuzi wa umma nchini.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments