Wanawake wanaoishi kwenye ndoa 137 kutoka maeneo mbalimbali nchini wamejitokeza kuomba msaada wa matibabu ya kupandikiza mimba (IVF) katika mpango maalum ulioandaliwa kwa lengo la kuwasaidia wanaokabiliwa na changamoto ya uzazi.
Akizungumza jana katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani Mshauri wa saikolojia ya masuala ya uzazi katika Hospitali ya Kairuki, Angel Pesha, alisema kuwa ndani ya siku nane za usajili zilizofanyika kuanzia Machi 5 hadi 12 mwaka huu, wanandoa hao walijitokeza kutoka maeneo mbalimbali ikiwemo Dodoma, Tanga, Zanzibar, Mbeya, Mwanza na Dar es Salaam.
Alifafanua kuwa mpango huo uliandaliwa na KGIVF kwa kushirikiana na kampuni ya Quality Medica Supply Limited, ukiwa na lengo la kuleta matumaini kwa wanandoa wanaoshindwa kumudu gharama za matibabu ya upandikizaji mimba.
Kwa mujibu wa Angel, baada ya kufanyika kwa mchujo wa awali, wanandoa 54 walikidhi vigezo vya msingi vya kushiriki katika mpango huo. Wengi wao wana umri wa kati ya miaka 35 hadi 40 na wenye kipato cha kati ya Shilingi 500,000 hadi 1,500,000 kwa mwezi.
Aliongeza kuwa baada ya kuchambua kwa kina vigezo mbalimbali ikiwemo hali ya kiafya, muda wa ndoa na kipato cha familia, wanandoa 26 waliingia hatua ya mwisho ya uteuzi.
”Kati ya wanandoa hao, asilimia 45.8 wamekaa kwenye ndoa kwa kipindi cha miaka 11 hadi 20 bila kupata mtoto au ujauzito, huku asilimia 54.2 wakiwa wamekaa kwenye ndoa kwa miaka 3 hadi 10, wengi wao wakiwa na kipato cha familia kisichozidi shilingi 500,000 kwa mwezi,” alisema.
Alisema mpango huo ni mwanzo wa kurejesha matumaini kwa baadhi ya wanandoa, ambapo kati ya waliobaki, wanandoa watatu wamechaguliwa kufadhiliwa matibabu ya upandikizaji mimba.
Angel, alisisitiza kuwa changamoto ya uzazi inaathiri watu wengi kimya kimya na mara nyingi huambatana na msongo wa mawazo pamoja na shinikizo la kijamii, hivyo ni muhimu jamii kuendelea kutoa msaada na uelewa kwa wanaopitia changamoto hiyo.
Katika hafla hiyo, mgeni rasmi Jokate Mwegelo aliipongeza taasisi ya Kairuki pamoja na wadau wake kwa kuanzisha mpango huo ambao unaleta matumaini kwa familia nyingi nchini.
Alisema juhudi za taasisi hiyo zinaonesha namna sekta binafsi inavyoweza kushirikiana na jamii katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.
Jokate alieleza kuwa yeye ni mdau mkubwa wa maendeleo ya wanawake na wasichana, hivyo aliona ni muhimu kushiriki tukio hilo ambalo lina lengo la kusaidia familia na hasa wanawake wanaokabiliwa na changamoto ya uzazi.
Aidha aliwahimiza wanawake kuendelea kushirikiana na kuondoa wivu usio na tija, akisisitiza kuwa umoja na mshikamano ni nguzo muhimu katika kufanikisha maendeleo yao.
Alitumia pia nafasi hiyo kuipongeza taasisi ya Kairuki kwa mafanikio yake katika sekta ya afya na elimu, akisema imekuwa mfano wa taasisi zilizoanzishwa na Watanzania na kuendelea kutoa huduma bora kwa jamii.
Akihitimisha, Jokate aliwahakikishia wadau wa mpango huo kuwa ataendelea kushirikiana nao katika kuhamasisha jamii kujua na kutumia huduma za matibabu ya uzazi zinazopatikana nchini, ili kusaidia familia nyingi zaidi kutimiza ndoto ya kuwa na watoto.


























