Wednesday, April 22, 2026
spot_img
HomeBiasharaTVLA Yatoa Elimu kwa Wauzaji wa Chanjo za Mifugo Kusini mwa Tanzania

TVLA Yatoa Elimu kwa Wauzaji wa Chanjo za Mifugo Kusini mwa Tanzania

Na Daudi Nyingo

Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), kupitia Sehemu ya Mipango, Masoko na Habari, imeendelea kutoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya chanjo za mifugo inazozizalisha kwa kufanya ziara maalum katika mikoa ya Mtwara na Lindi.

Ziara hiyo iliyofanyika kuanzia tarehe 20 hadi 22 Aprili 2026 ikiongozwa na wataalamu wa TVLA, akiwemo Afisa Masoko, Bw. Fihiri Mbawala pamoja na Daktari wa Mifugo, Dkt. Deogratus Kavishe.

Katika kipindi hicho, jumla ya maduka 32 yanayouza chanjo zinazozalishwa na TVLA yalitembelewa katika halmashauri mbalimbali za Mkoa wa Mtwara, zikiwemo Manispaa ya Mtwara, Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara na Halmashauri ya Mji wa Masasi.

Aidha, kwa upande wa Mkoa wa Lindi, ziara hiyo ilifanyika katika Manispaa ya Lindi pamoja na Halmashauri za Mtama na Nachingwea.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Bw. Mbawala alisema kuwa lengo kuu la ziara hiyo ni kuhakikisha wauzaji wanakuwa na uelewa sahihi kuhusu matumizi ya chanjo ili kuwasaidia wafugaji kupata matokeo bora na salama.

“Tunatoa elimu kuhusu namna sahihi ya kuhifadhi chanjo, usafirishaji wake, matumizi sahihi pamoja na tahadhari muhimu zinazopaswa kuzingatiwa ili kulinda ubora wa chanjo na afya ya mifugo,” alisema.

Kwa upande wake, Dkt. Kavishe alisisitiza umuhimu wa kufuata miongozo ya kitaalamu katika matumizi ya chanjo, akieleza kuwa matumizi yasiyo sahihi yanaweza kupunguza ufanisi wa chanjo au hata kuleta madhara kwa mifugo.

Baadhi ya wauzaji wa chanjo walioshiriki katika mafunzo hayo walieleza kufurahishwa na juhudi hizo za TVLA. Bi. Zakia Amri, muuzaji wa pembejeo za mifugo katika Manispaa ya Mtwara, alisema elimu hiyo imewasaidia kuongeza uelewa wao na kuboresha huduma kwa wateja.

“Awali tulikuwa hatuna uelewa wa kina kuhusu uhifadhi sahihi wa chanjo, lakini sasa tumepata maarifa yatakayosaidia kulinda ubora wa bidhaa tunazouza,” alisema.

Naye Bw. Juma Mgeni kutoka Wilaya ya Nachingwea alibainisha kuwa mafunzo hayo yameongeza imani kwa wateja wao.

“Wafugaji wanapopata maelezo sahihi kutoka kwetu, wanaamini zaidi bidhaa hizi na kuona matokeo mazuri kwa mifugo yao,” alieleza.

Ziara hii ni sehemu ya mkakati wa TVLA wa kuhakikisha chanjo zake zinatumika kwa ufanisi uliokusudiwa, sambamba na kuimarisha uhusiano na wadau wa sekta ya mifugo na kuongeza tija kwa wafugaji nchini.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments