Wananchi wa kata ya Magugu, Wilaya ya Babati mkoani Manyara, wameanza kunufaika na utatuzi wa mgogoro wa ardhi uliodumu kwa zaidi ya miaka 20, baada ya kupata uhakika wa makazi halali na mipaka rasmi ya maeneo yao.
Wananchi hao wamemshukuru Mkuu wa Wilaya hiyo kwa kufanikisha suluhu ya mgogoro huo uliokuwa ukihusisha uvamizi wa eneo la mwekezaji katika vijiji vya Malangi na Kirusix, ambako baadhi yao walikuwa wamejenga nyumba za kudumu na hata kuweka makaburi.
Katika juhudi za kumaliza mgogoro huo, Mkuu wa Wilaya alimshauri mwekezaji kukata sehemu ya eneo lake, hususan katika maeneo ambayo tayari yalikuwa yamekaliwa na wananchi wengi. Mwekezaji alikubali ushauri huo na kuachia sehemu ya ardhi ili wananchi waweze kuishi kihalali.




Hatua hiyo iliambatana na maelekezo kwa maafisa ardhi kwenda kupima eneo lililotolewa, kubaini ukubwa wake na kuweka mipaka rasmi kwa ajili ya matumizi ya wananchi.
Aidha, wananchi wote waliokuwa wamejenga katika eneo la mwekezaji walipangiwa viwanja katika eneo hilo jipya lililotengwa na kuhamishiwa rasmi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya aliwataka wananchi kuendelea kuishi kwa amani na kushirikiana katika kulinda mali za mwekezaji ili kudumisha uhusiano mzuri na kuhakikisha maendeleo endelevu katika eneo hilo.









