Walimu wa masomo ya Sayansi na Hisabati nchini wametakiwa kutumia teknolojia na mbinu bunifu katika ufundishaji ili kuongeza uelewa wa wanafunzi na kuchochea uzalishaji wa wataalamu watakaosaidia maendeleo ya taifa kiuchumi na kijamii.
Wito huo umetolewa Aprili 29, 2026 na Ofisa Elimu Mkoa wa Shinyanga, Samson Allute, wakati akifungua mafunzo ya siku tano kwa walimu wa Sayansi na Hisabati kutoka mikoa ya Shinyanga na Simiyu.
Amesema matumizi ya teknolojia yatawawezesha walimu kufundisha kwa ufanisi zaidi na kuwahamasisha wanafunzi kupenda masomo ya Sayansi na Hisabati tangu ngazi za awali.
Allute amesema Serikali inaendelea kuwekeza katika sekta ya elimu kupitia Mradi wa Kuboresha Elimu ya Sekondari nchini (SEQUIP), unaolenga kuboresha miundombinu ya shule, mafunzo kazini kwa walimu pamoja na matumizi ya TEHAMA.
Amesisitiza kuwa walimu wanapaswa kwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia ili kuwajengea wanafunzi uwezo wa kufikiri kwa ubunifu na kuwa wataalamu wa baadaye watakaosaidia maendeleo ya nchi.

Aidha, amewataka walimu kutumia mafunzo hayo kupunguza hofu kwa wanafunzi dhidi ya masomo ya Sayansi, ambayo kwa muda mrefu yamekuwa yakionekana kuwa magumu.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo, akiwemo Happiness Goyi, mwalimu wa Kemia kutoka Simiyu, wamesema mafunzo yatawasaidia kutumia mbinu za kisasa zinazorahisisha ufundishaji na kuongeza uelewa wa wanafunzi.
Naye Daniel David, mwalimu wa Fizikia, amesema matumizi ya teknolojia yatawasaidia wanafunzi kuendana na ushindani wa dunia ya sasa yenye maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Kwa ujumla, mafunzo hayo yanatarajiwa kuwajengea uwezo walimu 523 kutoka mikoa ya Shinyanga, Simiyu, Tabora na Katavi ili kuboresha matokeo ya wanafunzi kupitia ufundishaji wa kisasa.





