HomeHabari‎Bodi ya DAWASA yataka kasi utekelezaji wa miradi ya kimkakati

‎Bodi ya DAWASA yataka kasi utekelezaji wa miradi ya kimkakati


‎Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) wamewataka wakandarasi wanaotekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati kuongeza kasi ya kazi ili kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati na kuanza kutoa huduma iliyokusudiwa kwa wananchi.

‎Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya miradi hiyo, Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa DAWASA, Mhandisi Elizabeth Kingu, amesema Bodi inaendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi inayolenga kuboresha upatikanaji wa huduma za majisafi na usafi wa mazingira kwa wakazi wa Dar es Salaam na Pwani.

‎“Ziara yetu imeanza katika mtambo wa kisasa wa kuchakata majitaka wa Kisopwa, kisha tukatembelea miradi ya majisafi ya Bangulo na Golani na baadaye mradi wa usafi wa mazingira wa Mbezi Beach. Tumepokea taarifa za maendeleo ya utekelezaji wa miradi hiyo na kusisitiza umuhimu wa kuikamilisha kwa wakati,” amesema Mhandisi Kingu.

‎Ameongeza kuwa miradi hiyo ina mchango mkubwa katika kuboresha maisha ya wananchi, hivyo ni muhimu kuhakikisha utekelezaji wake unakwenda sambamba na malengo yaliyowekwa ili huduma zianze kutolewa kwa wakati.


‎Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Mkama Bwire, amesema Mamlaka inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati yenye lengo la kuongeza uwezo wa uzalishaji, usambazaji na upatikanaji wa huduma za maji pamoja na kuimarisha miundombinu ya usafi wa mazingira.

‎“DAWASA inaendelea kuwekeza katika miradi ya kimkakati ili kuongeza uwezo wa uzalishaji na usambazaji wa maji, kuboresha miundombinu na kutoa suluhisho la kudumu kwa maeneo yenye changamoto za huduma,” amesema Mhandisi Bwire.


‎Naye Diwani wa Kata ya Kunduchi, Mheshimiwa Michael Urio, ameipongeza DAWASA kwa utekelezaji wa Mradi wa Usafi wa Mazingira wa Mbezi Beach na kuomba katika awamu zinazofuata mradi huo uwafikie wakazi wengi zaidi.

‎“Awamu ya kwanza inanufaisha zaidi ya wakazi 11,000 katika maeneo ya Kawe, Kunduchi, Mbezi Juu na Wazo. Tunaomba maeneo yaliyobaki nayo yajumuishwe ili wananchi wengi zaidi wanufaike na huduma hii muhimu,” amesema Mhe. Urio.

‎Miradi hiyo ya kimkakati inatarajiwa kuongeza upatikanaji wa majisafi na salama kwa wakazi wa Dar es Salaam na Pwani, sambamba na kuimarisha huduma za usafi wa mazingira na kuunga mkono juhudi za Serikali za kuboresha ustawi wa wananchi.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments